DRC YAFURAHISHWA NA MIPANGO ENDELEVU YA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO NCHINI




●Yafurahishwa na Mifumo ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini

●Yapongeza BoT kununua tani 35 za dhahabu

●Yafurahishwa na Serikali kusaidia upatikanaji wa mikopo

NA MWANDISHI WETU, DODOMA 

Ujumbe kutoka Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa madini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FESOCOMIC) umeonyesha kufurahishwa na kuvutiwa na mipango mbalimbali endelevu inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya madini  katika kuwaendeleza na kuwainua wachimbaji wadogo nchini.

Hayo yalibainishwa jana Novemba 3, 2026, na Mwenyekiti wa FESOCOMIC, Alex Murusi, wakati akielezea kuhusu ziara ya ujumbe wa watu 17 kutoka DRC uliokuja Tanzania kujifunza namna ya kuendeleza sekta ya uchimbaji mdogo wa madini  kupitia wataalamu wa Wizara ya Madini na taasisi zake.

Katika kikao hicho Murusi alieleza kuwa, kwa kipindi kirefu FESOCOMIC imekuwa ikiona juhudi za Serikali ya Tanzania katika kurasimisha sekta ya uchimbaji mdogo, usimamizi wa masoko, udhibiti wa utoroshaji wa madini, utoaji wa mikopo na ruzuku kwa wachimbaji, pamoja na kuweka mipango ya  kuongeza utafiti kina wa madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo, haya ni  mambo yaliyowavutia kuja nchini kujifunza.

Murusi alifafanua kuwa, Tanzania imekuwa mfano bora barani Afrika katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kiuchumi na kiteknolojia.

Ujumbe huo ulipongeza mikakati ya Wizara ya Madini kupitia taasisi zake ikiwemo Tume ya Madini , Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kuweka mipango endelevu ikiwemo utafiti , mafunzo, leseni za ndogo za uchimbaji na  mitambo 15 ya uchoronga kwa ajili ya vijana na wanawake kupitia Programu maalum ya MBT.

Awali, akielezea kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini, Kamishna Msaidizi wa Madini anayesimamia Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), Terence Ngole, alieleza kuwa,  sekta ya madini kupitia uchimbaji mdogo imepata mafanikio makubwa ya kihistoria.

Ngole alisema kuwa, mchango wa wachimbaji wadogo katika mapato yatokanayo na Sekta ya Madini (maduhuli) unaendelea kukua kwa kasi na sasa umefikia asilimia 40. Kuhusu mchango wa sekta nzima kiuchumi, Ngole amefafanua kuwa kwa sasa sekta ya madini inachangia asilimia 10.3 katika Pato la Taifa (GDP).

Pamoja na mambo mengine, ujumbe huo utapata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya uchimbaji wa madini, vituo vya uchenjuaji, na viwanda vya uongezaji thamani (beneficiation) katika mnyororo mzima wa thamani wa madini nchini ili kujionea mifumo hiyo kwa vitendo.

Post a Comment

0 Comments