Na Victor Masangu,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amesema kwamba atowafumbia macho hata kidogo baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji ambao watabainika kuwa wao ndio chanzo kikubwa la chimbuko la kutokea kwa migogoro ya ardhi.
Nyongo ametoa kauli hiyo wakati wa kikao kazi cha kupitia andiko la mwongozo wa uwekezaji katika Mkoa wa Pwani kilichohudhuliwa na viongozi mbali mbali wakiwemo wakuu wa Wilaya,wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na viongozi wengine zikiwemo taasisi wezeshi.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa kukamilia kwa andiko la mwongozo wa uwekezaji utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwavutia wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali ya ndani na nje ya nchi.
Nyongo amesema kumekuwepo na baadhi ya migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Pwani ambayo mingine inachangiwa na wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji hivyo ameahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
"Tupo katika kikao hiki cha kupitia andiko la mwongozo wa uwekezaji Mkoa wa Pwani lakini kuna baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji wao ndio wamekuwa ni chimbuko la migogoro ya ardhi na kwamba wale wote watakaobainika tutawaondoa,"amebainisha Nyongo.
Aidha Nyongo amebainisha kwamba mwongozo huo wa uwekezaji katika Mkoa wa Pwani utakuwa ni mkombozi mkubwa sana katika suala zima la kuwekeza katika nyanja mbali mbali ikiwemo upatikanaji wa fursa za ajira.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa hakusita kuwahimiza wakuu wote wa Wilaya kuhakikisha wanapambana katika kuyalinda na kuyatunza maeneo waliyonayo ili yasiweze kuvamiwa na baadhi ya watu ili kuweza kuepukana na migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Shaibu Ndemanga amesema kwamba ana imani kubwa mwongozo huo wa uwekezaji katika Mkoa wa Pwani utaleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia wawekezaji mbali mbali.
Naye Mwenywekiti wa Halmashauri ya Kisarawe Idan Kitare ameupongeza mpango huo ambao utaweza kuleta tija zaidi hasa katika maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji.
Awali mkurugenzi mtendaji wa Taasisi huru ya utafiti wa sera za kiuchumi na kijamii nchini Tanzania (ESRF) Professa Fortunata Makene amesema mwongozo huo utasaidia kuchochea mageuzi makubwa katika fursa za ajira.
Mwongozo huo wa uwekezaji katika Mkoa wa Pwani pindi utakapokuja kuzinduliwa rasmi utakuwa ni mkombozi mkubwa katika kuwapatia fursa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali.

0 Comments