Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi)
NA ABRAHAM NTAMBARA
NAIBU
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Atupele Mwakibete ameliagiza
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuongeza juhudi ya utoaji wa
elimu ya Usalama Barabarani kwa umma, hususan shule za Msingi na Sekondari.
Pia ametoa maagizo kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoaja na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha kuwa Barabara zinatengenezwa, kurekebishwa na kuwekewa alama na michoro ya barabarani ili kuimalisha usalama kwenye baarabara hizo.
Waziri Mwakibete ametoa maagizo hiyo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambapo amesema kwamba mamlaka hizo zinapaswa kuzingatia taratibu na kanuni za kupunguza ajali.
Aidha amesema kwamba madereva wa magari na pikipiki wamekua ni sehemu kubwa ya vyanzo vya ajali kwa kuendesha kwa mwendokasi usioruhusiwa kisheria, kuyapita magari yaliyopo mbele bila kuchukua tahadhari, kutovaa kofia ngumu kwa wapanda pikipiki pamoja na kubeba abiria zaidi ya mmoja.
"Kupitia maadhimisho haya na wasihi watumiaji wote wa Barabara hususan madereva, abiria wapanda pikipiki na watembea kwa miguu kuzingatia kutumia ujuzi na elimu ya usalama barabarani tunayoipata kuonyesha mabadiliko kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za usalama barabarani, kuacha kushabikia mwendokasi kwa madereva na kutoacha watoto wadogo kutembea barabarani bila uangalizi,” amesema.
Aidha amepongeza juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kufanikiwa kupunguza ajali kwa kiwango cha asilimi 67 kwa kipindi cha mwaka jana huku akiliagiza jeshi hilo kuanzisha mfuko maalumu wakusaidia vifaa vya utendaji wa askari ili kupunguza ajali barabarani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salam Abduli Isango amesema kwamba kuna upungufu wa ajali za barabarani 368 kwa mwaka 2020 hadi 2021, ambapo mwaka 2021 zilitokea ajali 181 ukilinganisha na ajali 549 kwa mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimi 67.
Ajali za vifo zimeongezeka watu 15, kwa mwaka 2021 zilitokea ajali za vifo 74 ikilinganishwa na vifo vya ajali 59 zilizotokea mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 25.4, vilevile kuna upungufu wa watu waliojeruhiwa 401 kwani mwaka 2021 waliojeruhiwa walikua 176 ukilinganisha na majeruhi 577 katika kipindi Cha mwaka 2020 sawa na asilimia 69.4
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ACP Jumanne Muliro amesema kwamba jeshi hilo litahakikisha linawashugulikia kwa mujibu wa Sheria madereva wote ambao ni wagumu kusikia maelekezo ya usalama barabarani ili kuhakikisha matukio ya ajali za barabarani yanapungua.
|
0 Comments