Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa na Utafiti wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a, wakati alipotembelea ofisi ya uchakataji taarifa za hali za hali hewa, jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
NAIBU Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Ally Possi, ameitaka
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kubuni vyanzo vya mapato ambavyo ni
himiilivu na visivyoumiza washitiri ili kuisaidia taasisi kujiendesha na
kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango.
Naibu Katibu Mkuu Dkt.
Possi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Mamlaka hiyo na
kusema kuwa ongezeko la mapato litapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya
watumishi kuhama kwani mapato yataweka mazingira mazuri kwa watumishi.
“Nikupongeze sana
Mkurugenzi Mkuu kwani kazi yako inaonekana sababu utabiri kwa sasa ni wa
kuaminika kwa asilimia zaidi ya 80 lakini fikirieni kuja na vyanzo vya mapato
visivyoumiza washitiri wenu ili mtumie sehemu ya mapato hayo kama motisha kwa
watumishi wenu", amesisitiza Dkt.
Possi.
Dkt. Possi amesema kuwa
Serikali iko tayari kushughulikia changamoto zote zinazoikabili Mamlaka hiyo
ikiwemo changamoto za kuhama kwa watumishi ili kuhakikisha taasisi hiyo
inaendelea kuwa imara.
Ameongeza kuwa Serikali
itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa ili kuongeza uhakika wa
taarifa kwa kuwa sekta ya hali ya hewa inazitegemeza sana sekta nyingine
hususani za usafirishaji pamoja na kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, amemuhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa
Mamlaka imejipanga kikamilifu kuboresha miundombinu pamoja na kusomesha
watumishi ili kuendeleza weledi katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu-Uchukuzi, Dkt. Ally Possi yuko katika ziara ya kikazi
jijini Dar es Salaam ya kutembelea taasisi zilizo chini ya sekta hiyo ili kuona
shughuli mbalimbali za kiutendaji na kujadili namna bora ya kupata suluhu ya
chagamoto zinazowakabili.
0 Comments