RAIS SAMIA AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA KUTOKA UFARANSA KUJA KUWEKEZA TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na kuagana na mwenyeji wake Rais wa Ufaransa Mhe. Emmanuel Macron mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu ya Elysée, Paris nchini Ufaransa leo tarehe 14 Februari, 2022. PICHA NA IKULU

NA MWANDISHI WETU, UFARANSA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa kuwekeza Tanzania katika sekta za mifugo, kilimo, nishati, madini na maeneo mengine yenye fursa.

Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akilihutubia Shirikisho la Biashara la Ufaransa (MEDEF) mjini Paris, Ufaransa na kuongeza kuwa serikali yake inachukua hatua muhimu kuweka mazingira muafaka ya kukuza sekta binafsi.

Rais ameeleza kuwa Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi kwenye sekta binafsi kuhakikisha kuna wepesi wa kuanzisha na kufanya biashara nchini. 

Rais Samia amesisitiza kuwa jitihada za serikali yake zimeendelea kuleta matokeo chanya, kama vile kituo cha uwekezaji kimesajili miradi 256 mwaka 2021 inayotarajiwa kuzalisha ajira 53,025 na mtaji wa dola za kimarekani bilioni 3.749.

Wakati huo huo, nchi hizo mbili zimetia saini Hati ya Makubaliano kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na kampuni ya Kimataifa ya Bouygues Bâtiment kwa ajili ya ukarabati wa jengo la pili (Terminal II) la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Upande wa Tanzania katika hatua ya utiaji saini
ulifanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi - Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Ally Possi huku Ufaransa ukiwa umewakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kimataifa ya Bouygues Batiment (BBI), Bw. Eric Fleurisson.

Ufaransa unashika nafasi ya 35 kwa uwekezaji nchini Tanzania, ambapo tayari kuna miradi 40 yenye thamani ya dola milioni 73.4 za Marekani, na kuzalisha ajira 1,885 kufikia sasa.

Post a Comment

0 Comments