TRC YASAINI MKATABA UNUNUZI WA BEHEWA 1430 ZA MIZIGO


Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa (kulia) pamoja na  Kaimu Meneja wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Reng (kushoto) wakisaini mkataba wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2.
NA ABRAHAM NTAMBARA
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesaini mkataba wa ununuzi wa behewa 1430 za mizigo ya Reli ya Kisasa (SGR) ambao unagharimu Dola za Kimarekani milioni 127.2 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 300.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameiagiza TRC kuhakikisha inasimamia kwa uzalendo utengenezaji wa behewa hizo ambazo zitatengenezwa na Kampuni ya CRRC Inaternational ya nchini China.
Waziri Mbarwa amesema kwamba utengenezaji wa mabehewa hayo unapaswa kukamilika katika muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba, na kwamba TRC pamoja na timu itakayoenda nchini China kukagua na kusimamia utengenezaji huo inapaswa kuhakikisha mabehewa hayo yanakua na ubora unaotakiwa.
“Huu mradi unatakiwa ukamilike kwa muda uliopangwa naomba nitoe maagizo kwenu Bodi ya Wakurugenzi wa TRC na timu ya watu mtakaoenda China kuangalia utengenezaji wa mabehewa haya kuhakikisha mnafanya kazi hiyo kwa uzalendo behewa ziwe na kiwango cha ubora unaotakiwa, tunataka mradi huu ukamilike kwa haraka ili ujenzi wa reli unapokamilika mabehewa yawe tayari,” amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa akizungumzia mkataba huo, amesema kati ya behewa hizo 1430 zipo za kubeba mafuta, mifugo na magari.
Kadogosa ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa zitasaidia kukuza biashara nchini na nchi za jirani ikiwemo Uganda, Rwanda, Burudi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hivyo amesema zitarahisisha usafirishaji na kupunguza gharama za matengenezo ya barabara pamoja na ajali.
“Behewa za mifugo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha usafiri wa mifugo kutoka mikoa mbalimbali ya nchi kwenda kwenye masoko kwa haraka na salama,” amesema Kadogosa.
Naye Meneja Mkuu  Msaidizi wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Peng ameihakikishia TRC kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia makubaliano yakimkataba yaliyosainiwa  huku akiipongeza Tanzania kwamba endapo mradi wa SGR utakamilika utafungua milango yakiuchumi kwa nchi zingine za africa Mashariki.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa (kulia) pamoja na  Kaimu Meneja wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Reng (kushoto) wakionyesha mkataba waliosaini leo wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2.

Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame mbarawa akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ununuzi wa Behewa 1430 za mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China.

Post a Comment

0 Comments