Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea kwa niaba yake Bango lenye wa Anwani ya Makazi ya Ofisi ya Rais, Ikulu mara baada ya kuzungumza katika Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi kilichofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza
Mfumo wa Anwani za Makazi ili kurahisisha utambuzi wa wakazi na makazi katika
kuleta maendeleo endelevu nchini.
Rais Samia amesema hayo leo
tarehe 08 Februari, 2022 katika Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Mfumo wa
Anwani za Makazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete
Jijini Dodoma.
Rais Samia amesema lengo la
mfumo huo ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na Anwani ya Makazi katika
eneo lake analoishi, kaya, ofisi ama eneo la biashara ili kuweza kuhudumiwa kwa
ufanisi.
Aidha, Rais Samia amesema
mfumo huo wa utambuzi ni bora na unaendana na mabadiliko ya uchumi wa
kidijitali duniani hivyo ni muhimu katika zama hizi ambazo watu wanatumia
TEHAMA katika shughuli mbalimbali za mawasiliano kijamii na kibiashara.
Rais Samia amesema kuwa
kukosekana kwa mfumo wa uhakika wa utambuzi wa wakazi na makazi, kumekuwa na
athari nyingi za kiuchumi, kiusalama na kijamii.
Pia, Rais Samia amesema Mfumo
wa Anwani za Makazi una tija kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kuwezesha
kufanyika kwa biashara mtandao, kuimarisha ulinzi na usalama, kuongeza mapato
na kuongeza ajira.
Vile vile, Rais Samia amesema
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeshaandaa Postikodi
(anwani za kijiografia) na zimegawiwa kwa Kata zote nchini kwa ajili ya
kutambua makazi na hivi sasa wanakusanya taarifa za wakazi na kuweka
miundombinu ya majina ya mitaa na namba za nyumba.
Rais Samia ametoa wito kwa
Sekta zote nchini kuibua, kuwajengea uwezo na kuwatumia wataalamu watanzania
katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohitaji taaluma walizonazo kama
ilivyofanyika katika Programu Tumizi (Mobile
App) ya anwani za makazi.
Aidha, Rais Samia ameelekeza
Wakuu wa Mikoa kukamilisha zoezi la Anwani za Makazi kufikia mwezi Mei, 2022 na
zoezi hilo lifanyike kama operesheni maalum katika muda uliopangwa ikijulikana
kama Operesheni Anwani za Makazi.
Rais Samia amewatahadharisha
Wakuu wa Mikoa kuwa fedha za mradi huo sio za matumizi ya Ofisi (OC) bali ni
kwa ajili ya mradi huo na kuzitaka Halmashauri nchini kuchangia fedha kutoka
katika Halmashauri hizo na kuzitumia katika maeneo yao pamoja na kutumia nyenzo
zilizopo kutekeleza operesheni hiyo ili bajeti iliyotengwa na Serikali ikidhi
malengo ya operesheni hiyo.
Pia, Rais Samia ameelekeza
Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuwa fedha za mradi huo
zielekezwe kwa Wakuu wa Mikoa na kugawanywa kulingana ukubwa wa mikoa husika.
Vile vile, Rais Samia
ameielekeza Wizara hiyo kufuta kandarasi zote zilizopangwa kwa ajili ya
Halmashauri hizo na badala yake ziundwe Kamati maalumu ambazo zitasimamia
operesheni hiyo kama zilivyofanya katika ujenzi wa madarasa kupitia fedha za UVIKO
19.
Kwa upande mwingine, Rais
Samia ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha fedha zilizotengwa
kuwezesha Mfumo wa Anuani za Makazi zinatolewa kwa wakati na kuelekezwa kwa
Wakuu wa Mikoa ili kufanikisha mfumo huo ikiwa ni pamoja na bajeti ya kujenga
mkongo wa mawasiliano katika kila wilaya.
Rais Samia amesema Serikali
inafanya jitihada za kuwa na satellite
yake itakayoongeza nguvu katika mawasiliano ya mitandao ambayo
itawezesha kutunza kumbukumbu za kila mtanzania mwenye anuani ya mtandao.
Vile vile, Mhe. Rais Samia
amezielekeza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara
za Vijijini na Mijini (TARURA) kuzingatia Sheria zinazotaka kuweka majina ya
barabara katika barabara zinazojengwa na kuhakikisha kuwa kazi hiyo ni
endelevu.
Rais Samia ameitaka Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuendelea kuwashirikisha
wananchi na kuwapatia mafunzo katika ngazi za mitaa na vitongoji ili
kuhakikisha mradi huo muhimu wa Anwani za Makazi unafanyika na kuwahudumia
wananchi kwa ufanisi.
Aidha, Rais Samia amesema
utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya
nchi yetu na unapaswa kukamilika mapema ili kuwezesha zoezi muhimu la Sensa ya
Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti, 2022 kufanyika kwa
ufanisi.
0 Comments