Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam ACP Muliro Muliro
akiwaonyesha waandishi wa habari jezi bandia za timu ya Yanga Afrika 1208 ambazo
wamezibaini zinazotengenezwa na kusambazwa na kampuni ya GSM.
NA ABRAHAM NTAMBARA
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 17
kwa tuhuma za kuuza jezi bandia za timu ya Yanga Afrika 1208 zinazotengenezwa na
kusambazwa na kampuni ya GSM. Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Muliro amesema kazi ya
kuwakamata ilifanyika katika maeneo mbali mbali ya Jiji la Dar es Salaam, lakini
pia kwa kushirikiana na baadhi ya mikoa nchini kwa kipindi cha kuanzia Januari 2
hadi Januari 28 mwaka huu. “Katika Jiji la Dar es Salaam Jeshi la Polisi
limewakamata watuhumiwa watano, akiwemo Zahiri Hassan (17) Mmwera aliyekutwa
huko Uwanja Benjamin William Mkapa akiwa na Jezi bandia za Timu ya Yanga 52,
Kariakoo mtaa wa Agrey alikamatwa Majiba Ndahya (50) Msukuma akiwa na Jezi 124,
Mohamed Ramadhani (26) Mchaga alikutwa na Jezi 86, John Staslaus (19) Mchaga
alikamatwa na Jezi 39 na Emmanuel Kinasa (21) Msukuma alikutwa na Jezi 60,”
Amesema ACP Muliro. Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao waliwataja wenzao wa
Zanzibar, ambapo Uwanja wa Amani watuhumiwa watatu walikutwa na Jezi bandia 36.
Ameeleza kuwa Jezi zingine bandia 134 zilipatikana kwa kushirikiana na Polisi
Mkoa wa Tanga na Mwanza ambapo watuhumiwa tisa walikutwa na Jezi 811. “Jeshi la
Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linawatahadharisha wananchi wote
wanaojihusisha na vitendo vya kutengeneza, kuuza na kusambaza, bidhaa kwa kuiga
au kufananisha nembo za biashara au huduma za watu wengine iliyosajiliwa
kisheria, kufanya hivyo ni kosa na kinyume na sheria za nchi,” amesema na
kuongeza,. “Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka nyingine za kisheria ili
kuona watuhumiwa wamechukuliwa hatua kali za kisheria,”.
0 Comments