RC MJEMA AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MAENDELEO MAKUBWA ANAYOFANYA



Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akizungumza na wananchi mkoni humo jana wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo akihitimisha ziara yake.

NA ABRAHAM NTAMBARA, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Mjema ametoa kauli hiyo jana akizungumza na wananchi wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo akihitimisha ziara yake mkoani humo.

Amesema kwamba ndani ya kipndi cha mwaka mmoja cha uongozi wake Rais Samia ameweza kufanya maendeleo katika Sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya Barabara, Afya, Elimu na Maji.

“Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais kwa sababu ametuteremshia mvua ya maendeleo, tumepata mvua ya madarasa, tumepata mvua ya vituo vya Afya, tumepata mvua ya hospitali, tumepata mvua ya Barabara, tumepata mvua ya umeme, tumepata mvua ya Kilimo,” amesema RC Mjema.

RC Mjema amesema kwamba kuna watu ambao walidhani hayo hayawezi kufanyika lakini Rais Samia ameweza kufanya.

“Kwahiyo tuendelee kumpongeza Rais Samia kwa sababu amefanya yote haya na kuweka miundombinu vizuri kama hii nchi nzima. Kwa mkoa wa Shinyanga pia ile treni ya mwando kasi itapita hapa na kiwanja cha ndege pia,” ameongeza Mjema.

Aidha ameeleza kuwa hivi karibuni Rais Samia amepata tuzo kutokana na juhudi hizo anazofanya za kimaendeleo kwa ajili ya Watanzania.

“Huyu ni mwanamke shupavu, mwanamke jasiri, ni Rais ambaye anafikiria wananchi wake na Watanzania kwa ujumla. Kwa hiyo tunampongeza sana kwa hilo,” amesisitiza Mjema.

Kadhalika RC Mjema amempongeza Rais Samia kwa kuwa Miongoni mwa Viongozi 100 waliotajwa kuwa Viongozi wenye ushawishi duniani.

Amesema kwa kutambulika kwake duniani ni kwamba kila Mtanzania ametambulika.
Hivyo amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kwa sababu Rais Samia amejitambulisha na kuwatambulisha Watanzania duniani.

Aidha amesema katika maendeleo aliyoyafanya mkoa wa Shinyanga hauko nyuma kwani amewajengea Barabara/madaraja, vituo vya Afya, madarasa ikiwemo shule ya wasichana.


Post a Comment

0 Comments