ACT-WAZALENDO YAING’ANG’ANIA SERIKALI KUONDOA TOZO YA SHILINGI 500 KWENYE MAFUTA

Msemaji wa Sekta ya Nishati wa Chama cha ACT-Wazalendo Isihaka Mchinjita akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kuhakikisha inaondoa tozo ya shilingi 500 kwa kila lita ya Petroli, Diseli na mafuta ya taa ili kushusha zaidi bei ya mafuta hayo.

Pia, kimesisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwakuyawezesha mashirika ya TIPER na TPDC kununua na kuuza mafuta ili kuhakikisha unafuu zaidi unapatikana.

Hayo yamebainishwa leo Juni 2, 2022 jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Sekta ya Nishati wa Chama hicho Isihaka Mchinjita akieleza uchambuzi wa maeneo tisa kuhusu bajeti ya Nishati kwa mwaka wa Fedha 2022/23.

Mchinjita amesema mwenendo wa bei ya mafuta ya Petroli, Diseli na mafuta ya taa, umekuwa ukiongezeka kila mwezi tangu tarehe 01 Julai, 2021.

Kwamba kwa kipindi chote Serikali haikuwa inachukua hatua madhubuti za kuleta unafuu au kushusha bei hizo ili kuzuia kutokea kwa mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

“Bei za rejareja za mafuta ya Petroli, Diseli na mafuta ya Taa kwa mwezi Julai, 2021 ilikuwa shilingi 2,249 kwa kila lita ya Petroli, Diseli ilikuwa shilingi 2073 na mafuta ya taa ilikuwa shilingi 1,57,” amesema Mchinjita na kuongeza kwamba,

“Kupanda kwa bei hizi za mwezi Julai kutokea mwezi Juni, 2021 kwa sehemu kubwa zilichangiwa na sera za kikodi na sheria ya fedha ya mwaka 2021/22 ambayo ilifanya mabadiliko kwa ongezeko la tozo ya mafuta kwa shilingi 100 kwa kila lita moja ya mafuta ya Petroli na dizeli na kuongezeka kwa ada ya Petroli kwa shilingi 100 kwa kila lita moja ya mafuta ya taa. Ndio maana zilipelekea kuongezeka kwa bei hizo kwa shilingi 156 kwenye Petroli, Diseli iliongezeka shilingi 142 na mafuta ya taa iliongezeka shilingi 164,”.

Amesema kwamba ukilinganisha bei mpya zilizotangazwa juzi na kuanza kutumika jana tarehe 01 Juni 2022 ambazo zinaonyesha kuwa bei ya rejareja ya Petroli kwa Dar es Salaam ni shilingi 2,994 kwa lita, Diseli ni shilingi 3, 131 na mafuta ya taa shilingi 3,299 na bei za mwezi Juni, 2021 ambazo zilikuwa shilingi 2,249 kwa Petroli, Diseli shilngi 2073 na mafuta ya taa ni shilingi 1,957. Ongezeko la mwaka mzima ni Shilingi 745 kwa Petroli, Diseli shilingi 1058 na mafuta ya taa shilingi 1342.

“Kwa hiyo, kwa Mwenendo huu bado tunaona hali ni mbaya, wananchi wanaumia. Tunafahamu nafuu iliyopatikana kutokana na ruzuku ya Serikali ya Shilingi bilioni 100, lakini kama tulivyoona bado haitoshi. Sisi ACT Wazalendo, tumekuwa na msisitizo huo wa kuitaka Serikali iondoshe kodi ya shilingi 500 kwakila lita,” amesema na kuongeza,

“Tulitoa msisitizo huo tangu mwezi April ambapo bei za mafuta kwa rejareja zilikuwa shilingi 2861 kwa lita ya Petroli, huku Diseli ikiwa shilingi 2,692 na mafuta ya taa shilingi 2,682. Tuliamini kuwa kwa kuondosha tozo ya shilingi 500, ingeweza kuleta ahueni angalau kufikia bei zinazolingana na mwezi Julai na Agosti, 2021,”.

 Aidha, amesema azma ya Serikali kuweka miundombinu ya kuwa na hifadhi ya mafuta kimkakati itengewe fedha haraka kwa ajili ya utekelezaji.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments