ACT-WAZALENDO YAITAKA SERIKALI KUSITISHA UWEKAJI MIPAKA LOLIONDO


Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mapigano Loliondo.

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kusitisha mara moja zoezi la kuweka alama za mipaka (vigingi) katika vijiji vyote vinavyozunguka Pori Tengefu la Loliondo hadi Mahakama ya Afrika Mashariki itakapotoa hukumu.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 12, 2022 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapigano Loliondo.

Semu amesena kuwa Serikali inafahamu kuwa Juni 22 mwaka huu Mahakama ya Afrika Mashariki, iliyopo jijini Arusha itatoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na vijiji vinne mwaka 2017.

Ameleeza kuwa jitihada za wananchi wa Loliondo na Sale kutafuta muafaka wa eneo hilo, hazikukomea kutafuta mwafaka kwa kujadiliana na viongozi wa Serikali bali kwenye vyombo vya sheria.

“Mnamo Septemba 2017 vijiji vinne kati ya 14 vilifungua shauri namba 10 la mwaka 2017 dhidi ya Serikali ya Tanzania kupinga mlalamikiwa kuwahamisha kwa nguvu wafugaji, kuua mifugo, kuchoma moto nyumba, kutesa wanavijiji na kuwatoa katika ardhi ya vijiji vyao,” amesema Semu na kuongeza,

“Vijiji vilivyofungua kesi ni Ololosokwa, Oloirien, Kirtalo na Arash,”.

Semu amebainisha kuwa vijiji hivyo pia vilifungua shauri namba 15 la mwaka 2017 kuiomba Mahakama kuizuia Serikali kuacha kufanya jambo lolote katika eneo hilo hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Kwamba Septemba 25, 2018 Mahakama iliamuru Serikali kusubiri hukumu ya Kesi ya msingi.

Hivyo amesema kilichotokea jana na juzi ni dharau ya wazi kwa Mahakama kwamba Mahakama ya Afrika Mashariki ipo kwa mujibu wa Mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kudharau Mahakama ni kosa la jinai na inaharibu kabisa dhana halisi ya utawala bora,” ameeleza Semu.

Aidha Waziri Mkuu Kivuli, ameiraka Serikali kuunda Tume huru ya uchunguzi itakayokuwa na uwakilishi wa Jamii ya Kimasai itakayochunguza matukio ya vurugu zilizotokea Juni 10 mwaka huu.

Vile vile amewataka Maafisa na Askari waliohusika kuendesha operesheni iliyosababisha uvunjifu wa haki za raia wachukuliwe hatua za kinidhamu na washtakiwe.

Kadhalika ameitaka Serikali itumie njia ya majadiliano na ushirikishwaji ili kutafuta suluhu ya changamoto zote, hivyo Serikali ikae na wafugaji na wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo kutafuta suluhu.

Amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kusitisha azma ya kupandisha ardhi ya vijiji kuwa Pori la Akiba ili kulinda haki za wenyeji ambao ni ardhi yao.

“Na hili sio kwa Loliondo pekee bali kwa nchi nzima. Kwa mujibu wa Wildlife Conservation Act Na.5 ya 2009 sehemu ya 16 ilimtaka Waziri aondoe Mapori Tengefu vijijini,” amebainisha Semu

Post a Comment

0 Comments