TAMASHA LA ZIFF KUFUNGULIWA JUNI 18, 2022

Mratibu wa Tamasha la ZIFF Prof. Martini Muhando akizungumza jijini Dar es Salaam na Wasanii wa Bongo Movie, wadau na mabalozi wa nchi ambao  filamu zao zimebahatika mwaka huu kushiriki.




Matukio mbalimbali katika picha

NA ABRAHAM NTAMBARA

TAMASHA la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) linatarajiwa kufunguliwa Juni 18 na kilele chake kuwa Juni 26 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu wa Tamasha hilo Prof. Martini Muhando akizungumza na Wasanii wa Bongo Movie, wadau na mabalozi wa nchi ambao  filamu zao zimebahatika mwaka huu kushiriki.

“Tarehe 18 ndiyo itakuwa siku ya kufungua tamasha, na katika siku hiyo ya tamasha tutakuwa na filamu moja ambayo itakuwa inaonyeshwa ni filamu ambayo imevunja rekodi zote hapa Tanzania kwa filamu ambayo ilipendwa sana na sasa hivi inatembea nchi nzima. Filamu yetu ya kufungua tamasha letu mwaka huu ni ‘Vuta ni kuvute’,” alisema Prof. Muhando na kuongeza,

“Wote mnaifahamu ni filamu ambayo tunadhani itatuinua kidedea hapa duniani,”.

Hivyo Prof. Muhando aliwapongeza kina Dkt. Issa Shivji kwa kufanya filamu hiyo ambayo anaamini itakuwa bora katika Tanzania kwani ni nzuri na yakipekee kufanyika katika zama hizi.

Aidha alisema kwamba siku hiyo hiyo ya Juni 18 usiku kutakuwa na watu 15 au zaidi ambao watakuwa wakitokea Bagamoyo na kuelekea Zanzibar wakiwa  katika Jahazi.

“Nia yetu ni kwamba katika miaka hii ya kuanzia 2015 mpaka 2024, kwa miaka hii 10 ni miaka ya kusherehekea mchango wa watu weusi katika maendeleo ya Dunia, sasa Tanzania bado haijafanya chochote katika hilo, lakini sisi tukachukua nafasi hii ya kusema kwamba tunataka tuonyeshe ulimwengu kwamba sisi Waafrika historia yetu kwanza tunajivunia historia yetu, lakini vile vile tuko tayari kuchangia zaidi kwenye maendeleo ya Dunia,” alisema Prof. Muhando na kuongeza,

“Kwahiyo siku ya tarehe 18 usiku wataondoka watu 15 kuelekea Zanzibar, tutawapokea pale tarehe 19 asubuhi, wale wageni wetu ni wageni mchanganyiko Watanzania wazawa pamoja na Wamarekani Weusi ambao walihamia Tanzania baada ya kuona kwamba wametambua Afrika kama nyumbani kwao. Kwahiyo sisi tutawapokea pale kama watu huru,”.

Alisema kwamba mwaka jana kwa mara ya kwanza Serikali ya Marekani ilitambua kwamba hiyo ni siku muhimu sana kwa watu weuzi au kwa maana ya wenye asili ya Afrika waishio Marekani kwamba siku hiyo kila mwaka watakuwa wakifanya sherehe.

Prof. Muhando alisema kwa sababu wanatambua historia kati ya Zanzibar na watu waliopelekwa utumwani wameamua kwamba watasherehekea siku hiyo visiwani Zanzibar.

Kwamba baada ya sherehe hiyo, siku hiyo hiyo ya Juni 19 usiku wataendelea na uoneshwaji wa filamu nyingine, kwamba Juni 20 wataonesha filamu mchanganyiko pamoja na warsha kadhaa.

Alibainisha kuwa tamasha hilo litakuwa na jumla ya filamu 101 ambazo zinatoka nchi 33 kwamba hii inaonesha ni namna gani tamasha hilo ni la kimataifa.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments