Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Londo (Mb), amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini umedhamiria kikamilifu kumpeleka mwananchi wa kawaida katika uchumi wa kati.
Mhe. Londo amesema hayo wakati wa ziara ya kamati yake katika Kijiji cha Ilongero Wilayani Singida iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika Kijiji hicho.
Mhe. Londo amesema kupitia miradi inayotekelezwa na TASAF, Kamati yake ina uhakika itatoa ajira kwa wananchi wanaoishi katika kaya maskini, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kaya kwa ujumla.A
meongeza kuwa, lengo la Serikali kuzinyanyua kiuchumi kaya maskini kupitia TASAF ni kuhakikisha Tanzania ya Viwanda inaanza na wananchi wanyonge.“
Sisi kama wawakilishi wenu ambao tunafanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Rais ambayo imepewa dhamana ya kuisimamia TASAF, tunaahidi kuendelea kufanya nao kazi bega kwa bega ili kuhakikisha lengo la TASAF la kuboresha maisha ya kaya maskini nchini linatimia,” Mhe. Londo amesisitiza.K
wa upande wake, mnufaika wa TASAF wa Kijiji cha Ilongero Bi. Tabu Sima amesema ruzuku ya TASAF alipoipata kwa mara ya kwanza aliitumia kuchimba msingi wa nyumba yake anayoishi hivisasa.
Bi. Sima ameongeza kuwa, anaishukuru TASAF kwani ruzuku anayoipata imemuwezesha kusomesha watoto wake na kuendeleza biashara zake ambapo hata soko analofanyia biashara zake limejengwa na TASAF.
Naye Bi. Pili Mohamed mnufaika mwingine wa TASAF katika Kijiji cha Ilongero Wilayani Singida amesema, kabla ya kuanza kunufaika na TASAF alikuwa akiishi katika nyumba ya tope lakini mara baada ya kuanza kupokea ruzuku na kwa kupitia vikundi vya kuweka na kukopeshana walivyoanzishiwa aliweza kufyatua tofali `na kujenga nyumba bora anayoishi hivisasa.
Akizungumzia mchango wa TASAF katika Kijiji cha Ilongero, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, TASAF imefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kujenga mabwawa mawili pamoja na kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Kijiji hicho.
“Ni heshima kubwa kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutatua tatizo la maji kupitia mpango wa TASAF, ambalo lilikuwa likiwakabili wananchi wa Kijiji cha Ilongero kwa muda mrefu,” Mhe. Jenista ameeleza.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wako mkoani Singida kwa ziara ya kikazi ya siku mbili yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida.
0 Comments