NA MWANDISHI WETU
MFUKO wa SELF (Self Microfinance Fund) umefanikiwa kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa Shilingi bilioni 196.9 kuanzia 2021 hadi Juni 30, 2025 ili kuwawezesha wajasiriliamali na taasisi mbalimbali nchini Tanzania kupata mikopo kwa urahisi.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 15, 2025 na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Santiel Yona akizungumza katika kikao cha Wahariri na Waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa mikopo hiyo imewafikia wanufaika 1,83381, kati yao wanawake wakiwa 97,000 na wanaume wakiwa 86,000 na taasi 549 za kifedha.
Santiel amesema Mfuko huo umefanikiwa kutengeneza ajira 183,000 kwa Watanzania, kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na kutoa elimu ya fedha mara kwa mara kupitia makongamano, maonesho kama Nanenane na vyombo vya habari.
Kuhusu changamoto, amesema Mfuko wa Self umekutana na changamoto mbalimbali kama vile wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kifedha, wakopaji kutorejesha mikopo kwa hiari na wananchi wengi kujishughulisha na biashara zisizo rasmi.
Santiel ameongeza kuwa taasisi imeweka mipango mikakati ya kuwa na wanufaika 200,000 kwa kipindi cha miaka mitano (2025- 2030) kwa kutoa mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 300, kutoa elimu ya mikopo, kuongeza matawi kutoka 12 hadi 22 kufikia 2030, kuongeza ufanisi kwa kutoa huduma bora zaidi kwa teknolojia na uendelevu wa taasisi.
Akizungumzia kuhusu majukumu ya Mfuko huo, amesema ni kutoa mikopo, kutambua fursa zilizopo kwenye jamii, kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogowadogo, taasisi zinazopewa mikopo na kuwasaidia wajasiriamali wadogo kujiajiri.
"Sasa majukumu makubwa ya mfuko wetu ni nini, jukumu la kwanza ni kuhakikisha tunatoa mikopo na hii mikopo tunaitoa katika kategori tofauti tofauti, kwanza watu binafsi na taasisi ambazo zimesajiliwa na zinafanya kazi lakini jukumu la pili ni kuhakikisha kwamba wanazitambua fursa zilizopo katika jamii na jukumu la tatu ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo kufanya kazi na kujiajiri," mesema Santiel.
Mbali na majukumu hayo, Santiel amesema Mfuko wa Self unatoa huduma ya mikopo kwa wajasiriamali, taasisi zilizosajiliwa kisheria, watumishi wa umma na wakulima. Pia Self inatoa huduma za bima ili kuhakikisha huduma hizo za bima zinalinda mikopo inayotolewa.
Amebainisha kuwa mfuko huo una mpango wa kurahisisha huduma za mikopo kwa wajasiriamali wadogo na Watanzania kwa ujumla kwa kuongeza matawi mengi zaidi nchi nzima.
"Nia yetu ni kufungua matawi mengi zaidi kwa hiyo baada ya muda tutakwenda nchi nzima lakini kwa sasa hivi matawi hayo yapo kumi na mbili”, amesema Santieli.
0 Comments