Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo. Amewaomba kufungua maduka na kuendelea na biashara zao na kawahakikisha ulinzi.
Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam Namoto Yusuf Namoto akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgomo wa wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo.
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewaomba wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kufungua maduka na kuendelea na biashara zao na kawahakikisha ulinzi.
Chalamila amebainisha hayo leo Juni 24, 2024 alipotembelea soko hilo lilioko Wilayani Ilala Mkoani humo na kuzungumza na wafanyabiashara hao ambapo amesema atakayejaribu kuwafanyia vurugu wafanyabiashara waliofungua maduka yao, atashughulika naye.
“Nataka niwathibitishie yule atakayemletea mkwara aliyekubali kufungua, naapa mbele ya Mwenyezi Mungu, hapo ndipo nitakapoonyesha ‘show’ nzima. Kwa sababu mtu anakubali kufungua na wewe unamchimba mkwara, mimi ntakuchimba mkwara na hautainuka tena,” amesema.
Amebainisha kuwa badala ya kufanya mgomo na kufunga bishara zao wanatakiwa kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwani kero walizopelekwa Serikalini zinaendelea kushughulikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam Namoto Yusuf Namoto amesema malalamiko mengi yanayolalamikiwa na wafanyabiashara hao ni ya kisheria ambayo utatuzi wake ni lazima kupitia bungeni na kufanyiwa mabadiliko.
“Madai hasa hayajulikani ni nini kwani mengi walishakutana na Viongozi wakayaongea yanafanyiwa kazi ila kwa sasa Kuna vipeperushi vinavyosamba havionyeshi anuani ya muhusika hivyo ni ngumu kujua umuulize nani akupe haswa wanachotaka,” amesema Namoto.
Hata hivyo amesema kitendo cha kufunga maduka kinayumbisha uchumi wa nchi na kupoteza wateja hivyo ni vyema wakafungua maduka na kukaa mezani kwa mazungumzo.
Wafanyabiashara hao wamegoma, baada ya Jumamosi Juni 22, 2024 kusambaa vipeperushi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa mgomo huo utakaoanza leo.
Wafanyabiashara hao wamefunga maduka kwa madai ya kuchoshwa na vitendo wanavyofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Karikaoo, Martin Mbwana akizungumza na Mwananchi Juni 22, 2024 alikiri kuona vipeperushi hivyo, akieleza hiyo ni hasira za kuchoshwa na wanayofanyiwa na TRA.
0 Comments