BIASHARA SAA 24 DAR KUANZA RASMI FEBRUARI 22 MWAKA HUU, RC Chalamila asema Camera na Taa kufungwa kuhakikisha usalama


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema shughuli za biashara zitaanza kufanyika rasmi Kwa saa 24 mkoani humo kuanzia Februari 22 Mwaka huu.

RC Chalamila amebainisha hayo leo Januari 30, 2025 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema siku hiyo Kutakuwa na uzinduzi Maalum utakaoanzia Ofisini kwake hadi Kariakoo.

Hivyo amesema kuwa ili kufanikisha jambo hilo baadhi ya barabara zitafungwa na taa zitafungwa Kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama wa wafanyabishara na wananchi kwa ujumla.

"Mkoa Dar es Salaam ni muhimu kwenye ukuaji wa uchumi wa Nchi, hivyo Februari 22 mwaka huu tutazindua rasmi mpango wa shughuli za kibiashara kufanyika saa 24, kwa sasa tunaendelea kufunga taa za kutosha na maandalizi ya kufunga kamera yanaendelea vizuri kwa ajili ya usalama," amesema Chalamila.

Kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati uliofanyika Januari 27 hadi 28 Mwaka huu jijini Dar es Salama, RC Chalamila amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa ikiwemo kuimarisha amani, utulivu na usafi hivvyo ameelekeza wilaya zote kuendelea kusimamia suala la usafi ili Mkoa uendelee kuwa kivutio huku akisisitiza kuwa Serikali inakusudia kuanza kutumia usafiri wa treni na majini kuimarisha usafiri ndani ya jiji hilo.

Akizungumzia suala la ujenzi wa soko la Kariakoo Chalamila amesema zaidi ya bilioni 28 zimetolewa na Rais Dokta Samia Suluhu kwa ajili ya ujenzi wa soko  hilo na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 97 pia amesema kwa sasa bodaboda na bajaji hazijazuiliwa kuingia katikati ya jiji kwani walizuiwa kwa siku chache    kutokana na ugeni wa marais wa Afrika.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa bodi ya soko la kariakoo Hawa Ghasia amesema kuanzia januari 31 wanaanza kuweka majina ya wafanyabiaahara ambao walikuwepo kwenye soko la kariakoo kabla halijaungua ili wasajiliwe na kwamba baada ya hapo watasajili wafanyabiashara wapya na waliokuwa wanadaiwa wanapaswa kulipa madeni yao.

Post a Comment

0 Comments