Na Lydia Lugakila, Bukoba
WANANCHI wa Mkoa Kagera wametakiwa kuondokana na imani potofu na za kishirikiana kuhusu magonjwa ya mlipuko hususani marburg pindi yanapotokea ili kuweza kuwanusuru watu ambao bado hawajaona kuwa hili ni tatizo kubwa.
Hayo yalibainishwana Mkuu wa Mkoa huo hajjat Fatma Mwassa Januari 28, 2025 wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari zaidi ya 100 wa vyombo mbalimbali ili wapate elimu juu ya kuandika habari sahihi, wapate wapi taarifa sahihi zisizozua taharuki katika jamii juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Marburg yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali.
"Wananchi wengi hawaamini na wanapuuza kila kinachosemwa na wataalam, Watanzania tuna hulka ya kutoamini jambo hasa pale tunaposikia aliyeambukizwa ni mmoja au kufa ni mmoja yaani sisi kuamini kwetu ni mpaka wawe wamekufa wengi hii ni fikra potofu tena wengine wanafananisha na imani za kishirikiana tuache tufuate maelekezo yanayotolewa na wataalam," alisema RC Mwassa.
Alisema busara ni kukinga na siyo kusubiri kutibu, siyo kusubiri watu watu wadondoke bali kuwaelimisha watu wajikinge kabla hivyo akawataka waandishi kuhakikisha wanatoa elimu kwa ĵamii kupitia vyombo vyao vya habari jinsi ya kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa huu, hatari ambapo ametoa mfano kuwa wakiugua watu 10 tisa kati yao hufariki.
Alisema hivyo tunahitaji nguvu kubwa katika kufanya kampeni juu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama huu wa marburg pindi yanapotokea.
Alisema kuwa Marburg ilitangazwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 20 mwezi huu na kusema kuwa kipo kisa cha mgonjwa mmoja ambacho kimetokea wilayani Biharamulo hali ambayo imesababisha timu ya Serikali kupitia idara ya Afya na wadau mbalimbali kufika Wilayani humo na kuanza kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha ugonjwa huo hausambai na kuleta visa vipya.
Naye Mkurugenzi wa kinga toka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa, maumivu ya kuchwa, maumivu ya misuli, kuharisha, mwili kuishiwa nguvu, vidonda vya koo, vipelele vya ngozi, maumivu ya tumbo, kutapika, kutokwa damu sehemu mbalimbali za wazi mfano puani, kutapika damu na kuharisha damu.
Naye Dk. Norman Jonas ni mratibu wa huduma za Afya ngazi ya jamii kutoka Wizara ya Afya alisema ugonjwa wa marburg unasababishwa na virusi vya marburg na unaambukizwa kwa haraka kwa njia mbili ambazo ni kutoka kwa wanyama na kwa binadamu na binadamu kwenda kwa binadamu.
0 Comments