TANZANIA imepongezwa kwa kufikisha nishati ya umeme
hadi ngazi ya vijiji hali inayoendelea kuchochea maendeleo na ustawi kwa
wananchi vijijini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika
(AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina wakati wa mkutano wa nishati Afrika leo Januari
27, 2025 jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania ni
mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika kwa kufanya vizuri katika
uwekezaji wa miundombinu na miradi ya usambazaji iliyoiwezesha nchi hiyo
kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,318.
"Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Rais wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa Tanzania
kufikiwa na nishati ya umeme katika
vijiji vyote, jambo hili linastahili kupongezwa kutokana na umuhimu wa nishati
hii katika maendeleo," amesisitiza Dkt. Adesina.
Kuhusu mkutano wa Nishati Afrika Dkt. Adesina amesema kuwa lengo ni kuwafikishia umeme watu
Waafrika milioni 300 wanaoishi chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara akisisitiza
kuwa lengo hilo linakwenda kufanikiwa
akisisitiza uwazi na uwajibikaji.
"Mkutano huu unalenga kuifungua Afrika kwenye
eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika nchi za Afrika
wanaunganishwa na umeme,".
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia
Dkt. Situmbeko Musokotwane ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiuzia umeme
nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na upungufu wa nishati hiyo.
"Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa kutuuzia
umeme kwa sababu nchi yetu imekua na changamoto ya upungufu wa umeme", amesema
Dkt. Musokotwane
Mkutano wa nishati Afrika unafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Tanzania ukiwakutanisha wakuu wa nchi za Afrika kwa lengo la kuwafikishia nishati ya umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
0 Comments