Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo Dorothy Semu (picha ya kwanza juu) akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu Makao Makuu ya Chama Magomeni jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha ACT Wazalendo kimesema kitaunganisha nguvu na vyama vyote makini na wadau wa demokrasia nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinaondoka madarakani.
Hayo yamebainishwa leo Februari 23, 2025 na Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu Makao Makuu ya Chama Magomeni jijini Dar es Salaam.
"Tukielekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ni muhimu kutambua kwamba kuna hujuma na hila zinazotumiwa ili kukata tamaa wananchi. Hali hii inatufanya tuwe na jukumu kubwa la kusukuma ajenda ya kuunda jukwaa la mapambano ya pamoja na vyama makini," amesema Semu na kuongeza,
"Tunahitaji kufanya shughuli za pamoja ili kuimarisha umoja wetu wenye nguvu utakao leta tija ya mabadiliko. Tunahitaji kupambania kuurejesha uchaguzi. Nchi yetu hasa hakuna uchaguzi, tuna uchafuzi,".
Semu ameeleza kuwa CCM haitaki na haiwezi kushindana kwenye uchaguzi wa haki, huru na wa kuaminika.
Hivyo amedai kuwa uchaguzi unatawaliwa na mabavu ikiwemo vipigo, kamatakamata, utekaji na mauaji ya wanachama na wananchi wanaopinga wizi wa kura.
Kwamba viongozi, wanachama na wananchi wanaendelea kupoteza matumaini kutokana na mwenendo usioridhisha wa chaguzi nchini ambapo amedai kuwa CCM imekuwa ikipendelewa.
"Ni vizuri kukumbushana kuwa pamoja na hayo yote uchaguzi ni kama Vita. Vita ina majira yake. Kuna wakati wa faraja ya ushindi na kuna wakati wa majanga katika vita (casualities). Kuna wakati wa ari ya kimapambano kutokana na dalili ya ushindi au ushindi kwenye baadhi ya mapambano na kuna kipindi cha kuvunjika ari kutokana na kupoteza baadhi ya mapambano (battles)," ameeleza Semu na kubainisha,
"Wajibu wa jemedari mzuri ni kutambua hali halisi katika vita na kuchukua hatua stahiki. Jemedari hapaswi kukata tamaa, bali anapaswa kuchukua hatua stahiki kulingana na hali halisi. Chama chetu kipo katika hali ya vita inayotokana na mazingira yanayokatisha tamaa,".
Ameendelea kuzema "Wajibu wetu kama majemedari katika vita yetu ni kuhakikisha kuwa hatukati tamaa. Iwapo Wajumbe wa Halmashauri Kuu tutakata tamaa, hilo litakuwa ni tamko la kushindwa vita, jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu kutokea,"
Ameeleza kuwa Chama chao kinapaswa kujipanga vizuri kuhakikisha kuwa kinadhibiti hujuma za CCM na dola na kinafanikisha malengo yake ya kisiasa kama ambavyo majemedari hodari kwenye vita mbalimbali ulimwenguni waliweza kuusoma mwelekeo wa vita, kufufua ari ya mapambano na kusonga mbele hadi kuupata ushindi.
"Kwa mshikamano wetu, kwa hakika, tutayafikia malengo yetu. Ndugu zangu, ni wakati wa kuchukua hatua. Tuwe na mshikamano na umoja katika kukabiliana na matatizo yanayotukabili. Kwa pamoja, tunaweza kufanikisha malengo yetu na kuleta mabadiliko tunayoyahitaji," amebainisha Semu.


0 Comments