MADINI YENYE THAMANI YA SHILINGI ZAIDI BILIONI 1.3 YAKAMATWA KAGERA







●Ni Vipande 163 vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 4434.6

●Naibu Waziri wa Madini atoa onyo kali kwa mitandao inayojihusisha na biashara haramu ya madini

●Mpaka Machi 2026 madini yenye thamani ya bilioni 3.31 yamekamatwa

Na Mwandishi Wetu, Kagera

MAMLAKA za serikali nchini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vimefanikiwa kukamata  madini ya dhahabu yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.345,998,291.67 yaliyokuwa yakitoroshwa kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.

Kukamatwa kwa madini hayo kumeripotiwa kufuatia operesheni ya Julai 1, 2026 iliyofanywa na Jeshi la Polisi, Tume ya Madini  kwa kushirikiana na  vyombo vya Ulinzi na Usalama na  Kikosi Kazi cha Kuzuia  Utoroshaji wa Madini.

Baada ya utambuzi na uthamanishaji  kufanyika ilibainika kuwa  idadi ya vipande vya dhahabu vilivyokuwa vikitoroshwa ni 163  vyenye uzito wa gramu 4434.66.

Hayo yamebainishwa leo Julai 13, 2026 mkoani Kagera  na Naibu wa Madini Dkt. Steven Kiruswa  wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Dkt.Kiruswa amesema kuwa, Serikali imejipanga vyema kuendelea kusimamia Sekta ya Madini ili kukabiliana na  utoroshaji wa madini unaofanywa na watu ambao sio waaminifu nchini.

Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, katika kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026 , Serikali imefanikiwa kukamata madini yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.31 ambayo yalikamatwa katika matukio 55 nchini kote.

Dkt.Kiruswa ametoa wito kwa wachimbaji, wafanyabiashara wa madini (dealers na brokers), na wananchi kwa ujumla kutumia masoko rasmi zaidi ya 40 ya madini na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa kote nchini ili kufanya biashara zao kwa usalama, uhuru, na kuchangia maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments