MAPAMBANO 14 KUSHUHUDIWA MSIMU WA TATU WA KNOCK OUT YA MAMA, ni leo Februari 28, 2025




NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.

MSIMU wa tatu wa Knock Out ya Mama unaofanyika leo Februari 28, 2025 jijini Dar es Salaam utakuwa na mapambano 14 yakihusisha mabondia wa ndani na nje ya nchi ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anatarajia kuwa mgeni rasmi.

Kuelekea mapambano hayo jana kulikuwa na zoezi la kupima uzito na face-off kwa mabondia wanaotarajiwa kushuka ulingoni  katika mapambano ya raundi sita na nane, yakiwemo yale ya main event.

Katika tukio hilo lililofanyika Magomeni Sokoni, Mafia Boxing Promotion pia wametoa mitungi ya gesi kwa wanawake wajasiriamali ili kuwawezesha kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamasisha matumizi ya gesi kama chanzo safi cha nishati.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Mafia Boxing Promotion, Ally Zayumba, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia kama gesi na umeme badala ya kuni na mkaa.

Baadhi ya wanawake waliopokea mitungi hiyo walielezea furaha yao kwa hatua hiyo na kupongeza Mafia Boxing Promotion kwa kuona umuhimu wa kusaidia jamii na kuunga mkono sera ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu nishati safi ya kupikia.

Katika zoezi la kupima uzito, Rashid Matumla, bondia mstaafu na baba wa Amiri Matumla, ambaye anapigana kwenye main card, alisema kuwa mwanawe amejiandaa vizuri na ana nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya ulingo.

Kwa upande wake, Amiri Matumla aliahidi kutoa ushindi mnono dhidi ya mpinzani wake, Paulo Amavila kutoka Namibia, huku Amavila akijigamba kuwa Matumla bado ni mdogo kwake na hana nafasi ya kushinda.

Naye Promota mkongwe, J. Msangi, aliwapongeza Mafia Boxing Promotion kwa jitihada zao katika kuendeleza mchezo wa ngumi, akisema kuwa wao walifungua njia na sasa Mafia Boxing wanaendeleza kwa kiwango cha juu, huku akitabiri Tanzania kupaa zaidi kimataifa katika masumbwi.

Mashabiki wa ngumi wanatarajiwa kufurika Magomeni kesho kushuhudia mapambano makali na burudani ya kipekee.

Post a Comment

0 Comments