Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza na Wananchi (hawapo pichani) katika Soko la Tandika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
NA ABRAHAM NTAMBARA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewataka wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam kuhakikisha wanalinda amani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye Mwaka huu.
RC Chalamila amebainisha hayo leo Februari 12, 2025 akizungumza na wananchi wa Temeke katika siku ya pili ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa Serikali katika Halmashauri hiyo ambapo ametembelea Mradi wa Stendi ya Buza na Ukarabati wa Soko la Temeke.
Amesema kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu vyama vya siasa vitapita Kwa wananchi kutoa Sera zao, vipo vitakavyotumia fursa hiyo kuhubiri sisa za uvunjifu wa amani ya Nchi, hivyo amewataka wananchi kujiepusha na sisa za namna hiyo.
"Ndugu zangu amani ni kitu muhimu sana. Kuelekea Uchaguzi Mkuu vyama vya siasa vitapita kueleza Sera zao, wapo watakaohamasisha uvunjifu wa amani, hivyo tujiepushe nao, atakayejihusisha na uvunjifu wa amani hatavumiliwa," amesema RC Chalamila.
Akizungumzia kuhusu Mradi wa Stendi ya Buza amboa umekamilika huku Dala Dala zikiwa bado haijaanza kuitumia, RC Chalamila ameagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke kukaa pamoja na LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ili kuhakikisha Dala Dala zinaanza kuitumia Stendi hiyo haraka iwezekanavyo.
"Mradi huu ni mradi wa umma na umegharimu fedha nyingi, hivyo ni lazima uwe na manufaa kwa wananchi," amesema RC Chalamila.
Katika hatua nyingine RC Chalamila amewataka wafanyabiashara katika Soko la Tandika kutumia fursa ya kufanya biashara Kwa saa 24 ili kujiongezea kipato.
Hata hivyo katika kufanikisha hatua hiyo ya ufanyaji biashara Kwa saa 24 amemwagiza Mkurugenzi kuendelea kufunga taa katika Soko na kueleza kuwa baada ya ufungwaji wa taa zitafungwa Camera zitakazo saidia katika kudhibiti wahalifu.
Hata hivyo RC Chalamila ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kulipa Kodi pamoja na kutoa lisiti wa wateja wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda amesema kuwa wanaendelea kufanya maboresho ya miundombinu katika Soko la Tandika ikiwemo ufungwaji wa taa ili kufanikisha ufanyaji wa biashara Kwa saa 24.
DC Mapunda ametumia fursa hiyo kutoa maagizo Kwa madereva wa Dala Dala kuanza kufika katika Stendi ya Buza kama walivyokubalina.
0 Comments