TAKUKURU KINONDONI YAFUATILIA MIRADI YA BILIONI 2, ni ya Sekta ya Elimu na Ujenzi, miwili yakutwa na mapungufu


Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Christian Nyakizee akitoa taarifa kuhusu utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba Mwaka huu mkoani Dar es Salaam.

NA ABRAHAM NTAMBARA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefuatilia miradi mitano yenye thamani ya shilingi bilioni 2,808,572,124.

Hayo yamebainishwa leo Februari 6, 2025 na Mkuu wa TAKUKURU (M) Kinondoni Christian Nyakizee akitoa taarifa kuhusu utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024.

Nyakizee amesema kuwa miradi hiyo ilihusu Sekta ya Elimu na Ujenzi ambapo kati ya miradi hiyo, miradi miwili yenye thamani ya shilingi 144,800,000 imekutwa na mapungufu madogo madogo.

Kwamba wahusika wameshauriwa kurekebisha mapungufu hayo na ufuatiliaji  utafanyika kuhakikisha wameufanyia kazi ushauri uliotolewa.

"Vilevile, Mradi mmoja wa ujenzi wenye thamani ya shilingi 90,000,000 ulibainika kubadilishwa kazi iliyotolewa kibali awali. Kibali kilichotolewa kilikuwa ni cha kufanya ukarabati wa majengo ya madarasa," amesema Nyakizee na kuongeza,

"Badala yake wakaanzisha ujenzi wa madarsa mapya. Ni kosa la kisheria kubadili matumizi ya fedha bila kibali kutoka sehemu husika hivyo Ofisi inaendelea na ufuatiliaji wa kina wa suala hili,".

Kuhusu uchambuzi wa Mifumo, Mkuu wa TAKUKURU (M) Kinondoni Nyakizee amebainisha kuwa, katika kipindi husika wamefanya uchambuzi wa Mifumo ya uondoaji taka ngumu ngazi ya kaya na maeneo ya biashara katika Manispaa ya Kinondoni.

Kwamba wamefanya uchambuzi wa mfumo wa usimamizi na ukusanyaji mapato Kwa njia ya kielekroniki (POS) katika Manispaa ya Ubungo, uwasilishaji wa michango ya mifuko ya hifadhi ya Jamii Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Kadhalika wamefanya uchambuzi wa mfumo wa usomaji Mita na Ankara za Maji DAWASA Wilaya ya Ubungo, hivyo ameeleza kuwa Ofisi imepanga kufanya kikao na wadau ili kijadili kilichobainika na kuwekeana maazimio ya namna ya kudhibiti changamoto hizo.

Kuhusu warsha, amesema katika kipindi husika wamefanya vikao na wadau wa chambuzi wa Mifumo iliyofanyika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.

Kwa upande wa uelimishaji umma, Nyakizee amebainisha kuwa wamefanya Semina 62, miajadala ya wazi 02, mikutano ya hadhara 32, uandishi wa makala 03, vipibdi vya Redio/TV 06, kuimarisha klabu za wamipinga Rushwa 26 na Mdahalo mmoja.

Post a Comment

0 Comments