ELIMU YA MBOLEA YAONGEZA TIJA KILIMO CHA PAMBA SIMIYU


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.  Anamringi Macha akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Kilimo, Idara ya Maendeleo ya Mazao Samson Poneja walipotembelea ofisini kwake kueleza uwepo wao mkoani humo   kutekeleza  kampeni ya Mali Shambani tarehe 3 Desemba, 2025.

Wakulima wa kijiji cha Hinduki kilichopo Halmshauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani wa Simiyu wakifuatilia mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea  tarehe 3 Desemba, 2025 ikiwa ni utekelezaji wa  kampeni ya Mali Shambani yenye lengo la kutoa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo, kuhamasisha wakulima kupima afya ya udongo na kujisajili kwenye mfumo wa pembejeo za kilimo ili kunufaika na ruzuku ya mbolea na mbegu inayotolewa na Serikali.

NA MWANDISHI WETU

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, amesema, elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imekuwa nguzo muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa mkoa huo. 

Akizungumza na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi zake leo tarehe 03 Desemba, ofisini kwake Mhe. Macha amebainisha kuwa, uelewa huu umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa uzalishaji, hususan katika zao la pamba.

Ameeleza kuwa, hapo awali matumizi ya mbolea hayakuzidi tani 100 kwa mwaka, lakini kwa msimu wa 2024/2025 matumizi yameongezeka hadi kufikia tani 605. 

Aidha, usajili wa wakulima katika mfumo wa kidijitali wa pembejeo za ruzuku umeongezeka ambapo kwa mwaka 2024/2025 jumla ya wakulima 426,331  wamesajiliwa na kuwa na  namba za Mkulima  na hivyo kuifanya Simiyu kuongoza kwa usajili kwa Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake, Maria Joseph, mkulima wa mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Bukaginja, amesema elimu ya matumizi sahihi ya mbolea  aliyoipata imemsaidia kubadili mtazamo kuhusu mbolea.

“Kwa sasa natumia mbolea ya kupandia na kukuzia. Zamani nilipata takribani magunia 7 kwa ekari moja, lakini baada ya kutumia mbolea kwa usahihi, sasa napata kati ya magunia 30 hadi 35,” amesema.

Naye, Samson Poneja, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Kilimo Idara ya Maendeleo ya Mazao, amewahimiza wakulima kuendelea kujisajili kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku  na kupima afya ya udongo ili kubaini virutubisho vinavyohitajika.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha huduma za ugani ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya kupimia afya ya udongo kwenye halmshauri zote ikiwemo Halmshauri ya Wilaya ya Maswa ili kuwawezesha wakulima kutumia virutubisho sahihi kwa mazao yao na hivyo kuongeza tija na ushindani katika sekta ya kilimo nchini.

Post a Comment

0 Comments