ACT WAZALENDO KUPIGANIA KUREJESHWA KWA THAMANI YA KURA KWENYE CHAGUZI


Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa kipaumbele cha Chama hicho kwa sasa ni kupigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi hasa kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania kwenye chaguzi.

Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa Chama Mstaafu wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi katika Mikoa ya Kusini Operesheni ya Chama hicho iliyopewa jina la Operesheni Linda Demokrasia kwa kongamano lililofanyika katika Jimbo la Lindi Mjini leo tarehe 29 Machi 2025.

"Operesheni Linda Demokrasia maana yake ni nini? Maana yake ni kurejesha heshima ya kura kila Mtanzania. Kwa chaguzi tatu mfululizo thamani ya kura imepotea. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 hakukuwa na kura, takribani wagombea wote wa upinzani walienguliwa. Mwaka 2020 tuliona kwa mara ya kwanza kura feki zikozagaa hovyo barabarani. Mwaka 2024 wakafanya kama mwaka 2020" alisema Zitto Kabwe na kuongeza;

"Tunapigania thamani ya kuratasi ya kupigia kura. Karatasi za kupigia kura zisiwe kwenye mikono ya mabalozi, polisi au Maofisa wa Usalama wa Taifa. Mpiga kura aikute kwenye kituo na aiche kwenye kituo, isitoke nyumbani kwa mtu"

Ndugu Zitto amesema kuwa hoja kuu ya Operesheni Linda Demokrasia ni mageuzi katika Tume ya Uchaguzi ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

"Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe kama Omari Mapuri ambaye amewahi kuwa Mwenezi wa CCM inawezaje kutenda haki kwa watu wote? Sheria ya sasa ya Tume Huru ya Uchaguzi imeweka utaratibu kuwa angalau wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindani. Watu waombe na wafanyiwe usaili. Serikali ya CCM haitaki kutekeleza jambo ambalo wamelitunga wenyewe" alisema Zitto Kabwe.

Zitto Kabwe amesema kutokana na kuvurugwa kwa demokrasia nchini, matokeo yake ni kuporomoka kwa uzalendo miongoni mwa wananchi.

"Kwa wizi wa kura CCM wanadhani wanatukomoa CCM. CCM wanalikomoa Taifa. Mapenzi kwa Taifa yanaporomoka, watu hawajivunii tena Utanzania, wanavumilia kwa sababu hawana pa kwenda" Zitto Kabwe.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo Ndugu Isihaka Mchinjita amewahimiza wananchi kupambana kuhakikisha kuwa misingi ya demokrasia nchini inarejeshwa.

"Kulinda demokrasia ni wajibu namba moja wa raia. Raia wanapokosa uhuru wa kuamua nani awe kiongozi wao wanakuwa watumwa ndani ya nchi yao" alisisitiza Ndugu Mchinjita.

Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea na programu mbalimbali za Operesheni Linda Demokrasia ikiwemo Makongamano ya kufafanua dhana hiyo kwenye Mikoa mbalimbali na ziara kwa wadau mbalimbali wa demokrasia.

Imetolewa na Shangwe Ayo, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo.
29 Machi 2025.

Post a Comment

0 Comments