NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kumrejesha mikononi mwa wazazi wake mtoto wa kiume wa miaka 8 anayesoma shule ya Msingi Mbezi Ubungo Dar es Salaam aliyetekwa Machi 6 , 2025 na Stanley Dismas Ulaya (18) Mkazi wa Kata ya Nguruka Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 9, 2025 Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi SACP Muliro Jumanne Muliro amesema Machi,8, 2025 Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa na baadae kumjeruhi kwa risasi alipojaribu kutoroka chini ya ulinzi.
Kwamba hatua hiyo ilifikiwa baada ya Askari kujaribu kumstua kwa risasi za juu lakini alikaidi ikabidi apigwe risasi ya paja na kujeruhiwa hivyo yuko Hospitali Chini ya Jeshi la Polisi akipatiwa matibabu.
“Mtuhumiwa huyo alitekeleza tukio hilo
tarehe 06 Machi, 2025 wakati mtoto huyo aliposhuka katika daladala kabla ya kuingia katika geti la Shule alikamatwa na mtuhumiwa na kumpeleka hadi Bagamoyo Pwani ambako mtuhumiwa alikaa nae vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari kuipiga huku akidai pesa kwa vitisho ili amuachie na asimdhuru mtoto huyo na wasipotuma watafuta maiti,” amesema Kamanda
SACP Muliro amebainisha kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilifanya kazi kubwa ya ziada ya ufuatiliaji Machi 8, 2025 majira ya saa 01 :00 usiku baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay alijaribu kutoroka kwa kukimbia na kulazimika kumpiga risasi mguuni na kwenye paja na kufanikiwa kumzuia baada ya kutotii tahadhari za risasi zilizopigwa hewani awali wakati anakimbia ambapo alipelekwa hospitali Kwa matibabu akiwa na hali mbaya.
Kwa upande wake Mzazi wa Mtoto huyo Johnson Koranya amesema kuwa siku ya tukio hilo alimpeleka mtoto shuleni na kumuacha kituo cha gari karibu na shule lakini ilipofika jioni mtoto hakurejea nyumbani ndipo walipoanza kumtafuta.
Koranya amesema walipomtafuta mwalimu kumuulizia mtoto, mwalimu alimpatia namba ya mtu aliyekuwa akimsumbua akimtaka mzazi wa mtoto huyo.
Hivyo Koranya amesema baada ya kuwasiliana Kwa namba hiyo aliambiwa atume kiasi cha shilingi Milioni 50 ndiyo mtoto aachiliwe asipotuma atakuta maiti ambapo aliamua kweenda kuripoti kituo cha Polisi ili asaidiwe.
Ametumia fursa hiyo kulishukuru Jeshi la Polisi, Kwa kufanikisha mtoto huyo kupatikana akiwa hai na Afya njema.


0 Comments