UNDP YAHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI


NA MWANDISHI WETU

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesisitiza umuhimu wa ubunifu, matumizi ya teknolojia na uwekezaji katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya nishati na kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati kwa maendeleo endelevu.

Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) linaloendelea katika Ukumbi wa Mwandoro, Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere – Sabasaba, jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Nishati kutoka UNDP, Bi. Sayuni Mbwilo, alitoa mchango wake katika mjadala uliojadili maendeleo ya sekta ya nishati, fursa za uwekezaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuimarisha upatikanaji wa nishati.

Bi. Mbwilo alieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuendeleza sekta ya nishati na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za nishati zilizo bora, za uhakika na endelevu.

Kongamano hilo limewakutanisha viongozi, watunga sera, wataalamu, wawekezaji, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu, kuibua fursa za ushirikiano na kujadili mikakati ya kuendeleza sekta ya nishati pamoja na mchango wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Post a Comment

0 Comments