NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman (OMO), amesema nchi inaharibiwa na viongozi wengi wenye mamlaka ya maamuzi, kwa kutowatendea haki wananchi wanaowaongoza.
Othman ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kiongozi yeyote atakayesimama kwa ajili ya haki ya wananchi wake ataishi kwa amani maisha yake yote bila ya kuwa na hofu.
Othman ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akiwashukuru waumini wa dini ya kiislam, viongozi wa Serikali, Masheikh na Maaskofu waliohudhuria katika futari aliyowaandalia katika hoteli ya Peacock.
Amesema ni heri kuwaachia wahalifu 100 wenye makosa kuliko kudhulumu haki ya mtu mmoja asiyekuwa na hatia na kuwataka viongozi wa Serikali kujihadhari na watu wanaowazunguka kwa kuwa wengi wanawapotosha kutenda yasiyofaa.
Katika hafla hiyo ya futari viongozi mbalimbali wa dini walikuwepo na Mwenyekiti wa jukwaa la Wahariri Tanzania alipata nafasi ya kutuma salamu.
Kwa upande wa viongozi wa dini, Sheikh Ponda Issa Ponda, alimueleza Othman kuwa viongozi walio madarakani wameshindwa kuangalia sheria zinazokandamiza haki za binadamu hasa ucheleweshwaji haki mahakamani.
Sheikh Ponda alisema, kuna Watanzania wapo magereza kwa zaidi ya miaka 10 lakini serikali imeshindwa kuthibitisha madai yao kwa maelezo kuwa uchunguzi unaendelea.
Sheikh Ponda ametolea mfano masheikh waliokamatwa hivi karibuni kuwa wamekaa gerezani miaka 10 na wiki iliyopita waliachiwa huru na baada ya siku moja Serikali imewakamata na kuwafungulia mashitaka mapya wakati yale ya kwanza wameshindwa kuyathibitisha.
Kwa upande wake Askofu Emaus Bandekile Mwamakula, aliwataka viongozi wajitathmini kama ibada hii ya kufunga wanaitendea haki, ikiwa matendo ya watu kutekwa, Haki za raia kuzidi kuminywa na watu kuendelea kuishi katika hofu hakujapatiwa ufumbuzi.

0 Comments