*Ni katika adha ya maji, awataka Watumishi wa Umma kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa wakati
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakwamua wananchi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa kuweka jiwe la msingi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ikiwa ni uzinduzi wa
Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe
Katika uzinduzi huo uliofanyika mkoani Kilimanjaro Rais Dkt. Samia amesema, kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni ukombozi kwa wananchi katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.
Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro mara baada ya uzindua rasmi amesema, mradi huo umeongeza uwezo wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same-Mwanga kufikisha maji safi na salama kwa wananchi kutoka watu 50,615 hadi 300,000 kwenye vijiji 38 katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.
Aidha Rais Samia amezungumzia pia jitihada kubwa zilizofanyika kuukwamua mradi huo na kuhakikisha wananchi wanapata maji, na kusema, haamini katika kushindwa, na amewarai watumishi wa umma kuwa na moyo wa kupambana katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Hata hivyo Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha awamu ya pili ya mradi huo inatekelezwa kwa ukamilifu ili kuimarisha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Korogwe.
Sambamba na hilo, amesisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa sekta ya maji, hususan katika kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inakuwa endelevu katika maeneo ambayo miundombinu ya maji imefika.
Pia amewataka watumishi wa sekta ya maji kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa wakati na kulinda vyanzo vya maji ili kuwezesha Serikali kutimiza ahadi yake kwa wananchi.
*#KAZIINAONGEA*

0 Comments