CCM: Kina kazi ya kutumikia Wananchi si kutukana matusi majukwaani


Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi  kimesema  viongozi  wake  wana kazi ya  kufanya  Siasa Safi na utekelezaji kwa Vitendo  kunakotokana na  matakwa ya Sera zake  na kutumikia wananchi  bila kuwabagua.

Vile vile , CCM kimejipambanua kuwa  ndio chama pekee  Barani Afrika,  kinachoheshimu heshima na utu wa kila binadamu.

Katibu wa Kamati  Maalum ya NEC  Zanzibar  idara ya Itikadi,  Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, ameeleza hayo huku akisema upinzani  utaendelea kwa miaka mingi ijayo  kupata tabu  kushinda na  sera za CCM. 

Mbeto alisema Siasa ya CCM na sera zake hazibaki ndani ya vitabu, kwenye  makabati na katika  mabango , bali hutekelezwa kwa vitendo ili kuleta  maendeleo  yanayoshuhudiwa hivi sasa Vijiji na Mijini.

Alisema kuna Vyama kadhaa Barani  Afrika  ambavyo ni hodari kwa kutunga Sera na kuandika Ilani  za Uchaguzi  lakini  vinaposhika dola , hushindwa kutimiza wajibu kwa jamii . 

"Siasa na Sera za CCM  zinakwenda  sambamba na utekezaji kwa vitendo ili kuleta msukumo chanya wa  maendeleo.Wapinzani  wetu   ndipo wanapojikuta hawakubaliki  kwa  Wananchi"  Alisema Mbeto 

Aidha Mwenezi  huyo, alisema siku zote kadri mtu  akiitazama Tanzania,  aidha Bara au  Visiwani , kumekuwa na hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na utekelezaji  wa Sera za CCM. 

" Watendaji wa Chama na serikali za CCM kutwa kucha  huchemsha bongo na kufanya mambo  yasiende mrama.  Kuchanua kwa maendeleo nchini ni uthubutu wa  kubeba   dhima na dhamana ya utekelezaji  wa Sera " Alieleza 

Mbeto  alisema  kwa sababu hiyo, ndio maana wananchi  wanapohudhuria mikutano ya hadhara  ya upinzani , huwasikiliza  viongozi  wao wanavyotoa matusi na  jeuri  kisha  huwapuuza na kuondoka .

"ACT,  Chadema, CHAUMA  ,NCCR-MAGEUZI , Tadea na vingine  magari  yao  yanapita katika barabara zilizojengwa na Serikali za CCM .Hata wanapoumwa hutubiwa kwenye  hospitali zenye ,madaktari, dawa na vifaa tiba  bora " Alisisitiza 

Katibu  huyo  Mwenezi aliongeza kusema  ndio  maana viongozi wa Upinzani , wanapokuwa majukwani   hukwepa kuzungumzia ushindani wa sera ,badala yake hutupa  matusi ,kejeli na Siasa za  Ubaguzi.

Post a Comment

0 Comments