SAFARI YA KUZAA NA KUHAMA KWA NYUMBU YATUA FITUR HISPANIA


Na Mwandishi wetu.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake inaendelea kunadi vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania katika maonesho ya FITUR yanayoendelea nchini Hispania ambapo watu mbalimbali wakiwemo wananchi waliotembelea banda la Tanzania wameonekana kufurahishwa zaidi na tukio la kuzaliana na kuhama kwa nyumbu kutoka hifadhi moja kwenda nyingine (The Great Wildebeest Migration).

Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Utalii na Masoko NCAA, Mariam Kobelo, ameelezea wageni wanaotembelea banda hilo kuhusu tukio hilo muhimu katika ikolojia na la kipekee duniani kwa namna nyumbu jike wanavyoshika mimba na kuzaa kwa wakati mmoja katika eneo la tambarare za Ndutu, Ngorongoro kuzaa na hatimaye kuendelea na safari yao kuelekea Serengeti.

Ameongeza kuwa tukio la kuzaliana kwa nyumbu huanza mwezi Desemba hadi Machi kila mwaka katika eneo la Ndutu Ngorongoro, eneo hili ni salama zaidi kiulinzi, malisho, maji, mandhari, hali ya hewa, na virutubishi vinavyowawezesha ndama kukua na kuchangamka kwa haraka na pia kuna uchache wa wanyama wakali ambao huhatarisha ustawi wa viumbe vinavyozaliwa.

 Vilevile, udongo wa eneo la Ndutu una madini asilia yanayochangia nyumbu jike kutoa maziwa yenye virutubisho vya kutosha kwa ajili ya kunyonyesha, huku yakisaidia pia ukuaji imara wa mifupa ya ndama katika hatua za awali za maisha yao, alisema Kamishna Msaidizi Mwandamizi Kobelo.

Sambamba na kuelezea tukio la kuzaliana kwa nyumbu, alielezea kuwa NCAA imeendelea kunadi vivutio vingine ambavyo havijulikani sana kama vile mlima Loolmalasin, Mapango ya tembo na maporomoko ya maji Endoro, Engaruka, Mumba Shelter Rocks, Kimondo cha Mbozi na Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai kwa ujumla.

Katika maonesho hayo ujumbe wa Tanzania ulipata nafasi ya kuzungumza na Ofisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Bi. Eva Mashala, ambaye amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake katika kutangaza utalii nje ya nchi kupitia Maonesho mbalimbali na kuongeza chachukwa ongezeko la wageni na kukuza pato la Taifa. 

Pamoja naye Kamishna Kobelo ameambatana na Afisa Utalii Bw. Yohana Nkwamah.

Post a Comment

0 Comments