#KAZIINAONGEA
Meneja wa Kanda ya Kati kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Venance Mashiba, amesema kuwa kwa mwaka 2024, Mkoa wa Dodoma umevunja rekodi kwa kusajili miradi 46 ya uwekezaji kutoka kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa — idadi ambayo haijawahi kufikiwa hapo awali.
“Kuanzia Januari hadi Mei 2025, tumefanikisha usajili wa miradi 14. Hili ni jambo la kujivunia, kwani linaonesha namna kituo kinavyoendelea kupiga hatua katika kuhamasisha na kuhudumia wawekezaji,” amesema Meneja Mashiba.
Hayo ameyasema Juni 18, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo yalianza rasmi Juni 16, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2025.
Kwa upande mwingine, Mashiba amebainisha kuwa licha ya mafanikio ya mwaka 2024, TIC imejiwekea lengo la kusajili miradi 1,500 ifikapo mwisho wa mwaka 2025 — ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Aidha, amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo ili kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji pamoja na fursa mbalimbali zilizopo, hususan kwa Watanzania.
*#KaziNaUtuTunasongaMbele*

0 Comments