Na Ahmada John, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema ACT Wazalendo hakiwezi kuafiki ukweli wowote kati yake na CCM zaidi ya chama hichi kila wakati kudhani demokrasia ya kweli ni CCM kuondoka madarakani .
Pia kimekanusha hakuna waraka wowote au makubaliano yatakayofanyika kati ya CCM na ACT yanayotaja kugawana madaraka.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikaadi ,Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema kitendo cha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman, kuwalalamikia Doaspora huko Uingereza ni matumizi mabaya ya wakati.
Mbeto alisema makubaliano ya kimsingi kati ya CCM na ACT ni kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar yanayotajwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
Alisema si kweli kama kulikuwa na mpango wa kugawana madaraka kama inavyodaiwa na Othman au wakati wa Hayati Maalim Seif sharif Hamad alipokuwa Makamo wa Kwanza wa Rais SMZ .
"Hata ukisoma Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 hakuna kipengele chochote au Ibara ya katiba inayotaka kuwepo na kugawana madaraka SMZ " Alisema Mbeto .
Aidha, alisema hata walipokutana kati ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar Awamu ya saba, Rais Mstaafu Dk Amani Karume na aliyekuwa kiongozi wa upinzani ,Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, hakukuwa na kabrasha la makubaliano yoyote ya aina hiyo.
"Makubaliano ya msingi ni baada ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kukiondoa kipengele cha katiba ya Zanzibar kilichosema anayeshinda achukue vyote na kutajwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar "Alieleza
Mbeto alisema mjadala wa kugawana madaraka Zanzibar, haukufikia tamati toka katika mazungumzo ya kupata suluhu yaliofanyika Bagamoyo Mkoa wa Pwani ambapo Wajumbe wa CUF walisusia mazungumzo hayo.
"Mazungumzo yaliogusia kutaka kugawana madaraka ni kati ya CCM na CUF si na ACT Wazalendo. Hata hivyo mazungumzo hayo yalikufa baada ya viongozi wa CUF kuikimbia meza ya upatanishi "Alisema Mbeto
Katibu huyo Mwenezi alisema viongozi wa CUF walipokimbia mazungumzo hayo ,baadae Dk Karume na Maalim Seif wakakutana faragha ikulu Novemba 9 mwaka 2009 na kufikia muafaka usio na maandishi .
"OMO hayajui yaliofikiwa kwakuwa wakati huo hakuwa mwanachama wa CUF wala ACT. Anahadithiwa na kupotoshwa na wanaompa taarifa hizo . Aonyeshe kabrasha la makubaliano yaliofikiwa kati yake na Rais Dk Mwinyi au na Maalim seif "Alisisitiza Mbeto.

0 Comments