MBETO ASEMA KUMZUIA RAIA YEYOTE ASIPIGE KURA NI KOSA LA JINAI



Na Mwandishi  wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi kimesema raia kutopiga kura kwa hiari yake si kosa la jinai bali akitokea mtu ,chama au kikundi kinachowazuia watu  wasipige kura hilo liitakuwa ni kosa la jinai.

 CCM kimesisitiza kuwa hiari ya mtu kutopiga kura ni uamuzi  wake ambao haukiuki wala kuvunja katiba na sheria.  

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar  Idara  ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto  Khamis ameeleza hayo  na kusema kila mwananchi aliyetumiza masharti ya sheria  ana haki ya kupiga kura.

Mbeto  alisema kwa mujibu wa Katiba ya Mwaka 1977 Ibara ya 74 chini ya sheria ya Uchaguzi  Namba  2 iliofanyikwa marekebisho mwaka 2024 ni kosa kumzuia mtu asipige  kura .

Alisema haki ya kupiga kura ni ya kila mtanzania aliyetajwa kwa haki za kiraia hivyo  ana wajibu wa kujiandikisha na kuwa mpiga kura.

"Kupiga  kura ni  haki ya kila raia katika Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania. Kutopiga kura ni hiari ya mtu lakini mtu au watu wakimzuia raia asipige kura hilo litakuwa ni kosa la jinai"Alisema Mbeto 

Aidha, Katibu  huyo Mwenezi  alisisitiza kuwa kuunda genge ,kundi au mtu kuamua kuzuia watu wanaotaka kupiga  kura hilo ni kosa la jinai, ingawaje mtu  ikiwa hataki kupiga  kura hatakabiliwa na jinai .

Hata hivyo Mbeto aliwahimiza wananchi waliojiandikisha katika Daftari  la Kudumu  la Mpige kura kujiandaa na Uchaguzi  wa oktoba mwaka huu.

"Hayupo na wala hatokeo mtu mwenye jeuri au ubavu wa kuzuia uchaguzi  usifanyike. Uchaguzi wa nchi umetajwa na sheria  na katiba ya nchi "Alisema Katibu huyo

Post a Comment

0 Comments