MNEC MWASELELA AWATAKA UVCCM SENETI YA VYUO NA VYUO VIKUU KUTANGAZA MAZURI YALIYOFANYWA NA RAIS SEMIA, awahimiza kuwajibu kwa hoja wapotoshaji






NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), kutoka Mkoa wa Mbeya Ndele Mwaselela, amewataka Wanafunzi Idara ya UVCCM Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu kuwa mabalozi wa kuitetea na kuisemea vyema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mwaselela ametoa kauli hiyo Juni 13, 2025 jijini Dar es Salaam akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima katika Kongamano la Uongozi Bora, Uchumi Imara na Siasa shirikishi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 lilikwenda sambamba na hafla ya kuwaaga wanafunzi wa zamani na kuwapokea wapya katika tawi la CCM katika Taasisi hiyo.

Amewataka wanafunzi hao kutambua nafasi yao kama vijana katika kuelezea mafanikio ya Serikali na kujibu hoja za wapinzani wanaopotosha taarifa za miradi ya maendeleo katika mitandao ya kijamii.

"Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi. Ni wajibu wetu kutambua malengo ya Chama Cha Mapinduzi kushika dola kupitia ridhaa ya wananchi kwa njia ya kura," amesema Mwaselela. 

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mwaselela amesema kuwa CCM ina uhakika wa ushindi kwa kuwa imepeleka maendeleo kwa wananchi, hivyo hakuna sababu ya kunyimwa kura.

Akieleza juu ya malalamiko ya vyama vya upinzani, Mwaselala amesema "Kelele zipo, na haziwezi kuzuiwa. Hata katika familia ya watu kumi, wawili lazima walalamike na wanane unakuta wako sawa." 

Amefafanua kuwa tofauti za kisiasa ni jambo la kawaida, lakini hilo halipaswi kuzua taharuki kwani maendeleo yanaendelea.

Aidha, Mwaselela amesisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa na kwamba CCM itashiriki kikamilifu kama ilivyo desturi yake.

Akihitimisha hotuba yake, Mwaselela alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonyesha uongozi madhubuti kwa vitendo na kuhakikisha amani, utulivu na maendeleo ya nchi vinaendelea kuimarika.

"Rais wetu ni mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno. Tumeshuhudia kazi kubwa anayoifanya kwa taifa letu. Kazi yetu kubwa kuonesha kazi zilizofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kujibu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu mitandaoni na ukweli usiopingika ni kwamba CCM tutashinda kwa kupigiwa kura maana kazi zilizofanywa zinaonekana," amesisitiza.


Post a Comment

0 Comments