KAMISHNA KUJI ATAKA UBORESHAJI NA UWAJIBIKAJI ILI KULINDA MALIASILI


KAMISHNA KUJI ATAKA UBORESHAJI NA UWAJIBIKAJI ILI KULINDA MALIASILI

#KAZIINAONGEA

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA (T) Musa Nassoro Kuji, amewaelekeza Maafisa na Askari wa Mikumi kuongeza uwajibikaji na utendaji kazi ili kuimarisha ulinzi wa maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hayo ameyasema hivi karibuni katika kikao kazi kilichofanyika Makao Makuu ya Hifadhi, Kikoboga. Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, maarifa, nidhamu, utii na ubunifu kufanikisha malengo ya Shirika na Taifa kwa kulinda maliasili.

Amewahakikishia kuwa Shirika linaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuboresha mazingira ya kazi, huduma za afya na motisha ili kuongeza ufanisi na ustawi wa maisha yao.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, John Nyamhanga, Mkuu wa Kanda ya Mashariki, ameeleza mikakati ya kuimarisha ulinzi wa maliasili na kukuza utalii.

Amesema doria zinafanyika ndani na pembezoni mwa hifadhi, zikiwemo za kudhibiti wanyama wakali, waharibifu na kushirikisha jamii.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Massesa, Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, alimkaribisha Kamishna Kuji na kuwasilisha taarifa ya utendaji.

Ameeleza kuwa watalii wameongezeka pamoja na mapato. Julai 2024 hadi Juni 29, 2025, hifadhi ilipokea watalii 174,433, ongezeko la 11.74% ikilinganishwa na matarajio ya 156,100. Ni ongezeko la 25.63% kutoka 138,844 wa mwaka 2023/2024.

Askari Uhifadhi Mkuu Okoth Mubaso amemshukuru Kamishna Kuji kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kuchapa kazi kwa weledi, nidhamu na kufuata maelekezo ya viongozi ili kuimarisha uhifadhi na shughuli za utalii.

Mikumi ni miongoni mwa hifadhi 21 chini ya TANAPA. Hufikika kirahisi kutoka Morogoro, na huvutia watalii kutoka Dar es Salaam, Dodoma na Pwani kupitia usafiri wa SGR.

*#KazinaUtuTunasongaMbele*

Post a Comment

0 Comments