BODI YA USHAURI TARURA YAIPA HEKO SERIKALI UJENZI DARAJA LA MOHORO, TARURA kuendelea kuondoa vikwazo vya miundombinu



*Wananchi waaswa kutunza miundombinu ya daraja

Rufiji, Pwani

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Florian Kabaka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha Wakala huo kutekeleza ujenzi wa daraja la Mohoro lenye urefu wa Mita 100 wilayani Rufiji.

Mhandisi Kabaka ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea ujenzi wa daraja hilo pamoja na ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Km. 4 zinazojengwa katika mji wa Ikwiriri wilayani humo.

“Niipongeze serikali kwa uwezeshaji huu kwa TARURA, kwakweli uwepo wake hata wananchi wanaishukuru kwa kufungua miundombinu kila mahali, nitoe heko kwa serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa TARURA pia nitoe heko kwa menejimenti ya TARURA kwa usimamizi”.

Aidha, amewataka wananchi wa eneo hilo kulitunza daraja hilo pamoja na vifaa vyote vinavyozunguka, pia kutochezea tuta la daraja hilo kwani linaenda kuleta uhakika wa mawasiliano yao kwa mwaka mzima hususan kipindi cha mvua.

“Daraja hili linaenda kuwaondolea shida iliyodumu kwa miaka mingi lakini kuwafungulia fursa ya kujenga uchumi wao na Taifa kwa ujumla”.

Ameongeza kusema kuwa TARURA inaendelea kuondoa vikwazo vya usafiri na usafirishaji kwa kuongeza mtandao wa barabara ili wananchi waendelee kupata huduma na kufanya kazi za kuinua uchumi wa watanzania.

Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji amesema kuwa mradi huo unaenda kuwasaidia wananchi kwani shughuli nyingi za ukanda huo ni uchumi wa blue pamoja na kilimo cha mazao mchanganyiko hivyo kukamilika kwa daraja hilo kutaondoa vikwazo kwa wakazi wa Mohoro.

Wakati huo huo Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Emmanuel Mahimbo amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 48 ambapo wameshakamilisha ujenzi wa boksi kalavati mbili, nguzo nne na sasa wanaongeza nguzo nyingine. 

Ameongeza kuwa mpango kazi wao wa sasa hadi kufikia mwezi Januari 2016 wawe wamekamilisha sehemu ya daraja ili wabaki na kazi ya kukamilisha barabara hivyo ili kwenda na kasi hiyo, Mkandarasi ameanza kuingiza mashine na kuongeza watumishi ili kwenda na wakati.       

Post a Comment

0 Comments