NA MWANDISHI WETU, RUFIJI
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi kutoka Jumuiya ya Wanawake (UWT), Wilaya ya Rufiji wamehoji ukimya wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) juu ya hatua waliyochukua baada ya kuwakamata na kuwahoji baadhi ya wajumbe wa Jumuiya hiyo Wilaya, waliotuhmiwa kujihusihsa na rushwa kwa ajili ya kumbeba mmoja wa wagombea wa viti maalum.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina wanachama hao, walieleza kuwa Julai nne mwaka huu,baadhi ya wajumbe wa kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Rufiji,walikamatwa na kuhojiwa na maafisa wa kuzuia na kupambana na rushwa, Takukuru wilaya Rufiji.
Walisema maofisa wa Takukuru Wilaya ya Rufiji walipata taarifa za utoaji rushwa,kufuatia baadhi ya wajumbe katika kata za Kipugila,Mwaseni na Mkongo,kutokupata kanga na fedha zilizodaiwa zimetoka kwa mmoja wa wagombea wa viti maalum ambaye mumewe ni Kigogo katika moja ya wizara nchini.
Chanzo hicho kilieleza kuwa fedha na nguo hizo,zilitoka kwa mke huyo wa Kigogo zikiwa zinagaiwa kwa wajumbe wa UWT wa kata mbali mbali katika jimbo la Rufiji,ikiwa ni kilainishi kwao wakati wa kupiga kura za mtu atakayepitishwa na CCM kwa nafasi hiyo kutoka mkoa wa Pwani.
Aidha chanzo cha Habari hizi zimeendelea kueleza kuwa mgao huo ulikuwa ukifanyika chini ya maelekezo ya mwenyekiti wa UWT Wilaya Rehema Ally Mlawa,ambaye ni miongoni mwa waliohojiwa na Takukuru Wilaya siku hiyo ya Julai 4, 2025.
“Wale wajumbe wa kata za Mwaseni,Kipugila na Mkongo,hawakupata kitu na ndiyo wakaanza kupiga simu kwa fujo,suala hili katibu alikuwa hajui na hata walipokuja kuchukuliwa na Takukuru kwake lilikuwa jambo geni”kilieleza chanzo chetu.
Mwingine aliyehojiwa na Takukuru na kukataa kusema sababu za kuhojiwa ni pamoja na Mwajabu Makarani,aliyedaiwa kufika na kanga za rushwa katika kikao hicho cha kamati ya Utekelezaji kilichofanyika Julai 4, 2025.
Kwa nyakati tofauti Makarani na Mlawa walipozungumza na gazeti hili Julai 6,walikiri kuitwa na baadhi yao kuzuiwa na Takukuru hadi siku ya Jumamosi,Julai 5 kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mlawa wakati akiongea na Mwandishi wa Habari hizi kwa njia ya simu,alitaka kujua sababu ya kutafutwa kwake,na alipoelezwa kuwa ni juu ya watu waliokamatwa akamalizia kwa kuhoji “ni wale wa UWT waliokamatwa na Takukuru?.
Alipoelezwa kuwa lengo ni kupata taarifa zao,akaomba aonane na waandishi moja kwa moja badala ya kuzungumzia kwenye simu jambo hilo.
Hata hivyo wakatu huo waandishi walipomfikia akaeleza kuwa jambo hilo lipo juu ya uwezo wake na kwamba atafutwe katibu wa CCM Wilaya kwa ajili ya kulizungumzia.
Kwa upande wake Makarani alisema waliruhusiwa baada ya mahojiano ya siku mbili, na kwamba muda huo hawezi kulizungumzia kwa kuwa anashughulika katika ugawaji wa chakula katika eneo la Mohoro na kuomba atafutwe baadae.
Baadae Makarani alipotafutwa alieleza kuwa anashindwa kuelezea kwa sababu kuna baadhi ya vitu anapaswa amuachie Mwenyezi Mungu na kuukosea uongozi na kuomba kukutana na mwandishi wa Habari hizi akihofia kuongea kwenye simu na nafasi yake ya uongozi haimruhusu.
“Ninyi mmeshajua kuwa tumeitwa kule kama viongozi mtajua nini cha kufanya mimi wacha nimuachie Mungu,maana mpaka sasa sijajua taarifa zangu kule zikoje na siwezi kuzungumzia hili kwenye simu”alisema wakati huo.
Katibu wa UWT Wilaya ya Rufiji,Mariam Mgasha,alisema ni kweli wajumbe wa kamati ya Utekelezaji wilaya waliitwa na Takukuru kwa ajili ya Mahojiano juu ya utoaji wa Rushwa.
“Mimi kukupa ABC ninakosea bwana haya mambo kama unataka stori yote inabidi uende kule kule Takukuru walipohoji mimi kukupa ABC ninakosea msemaji wa mwisho ni takukuru,mimi nimehojiwa aliyekutwa na hilo jambo amehojiwa na wamehojiwa watu tofauti tofauti”alisema.
Aliongeza kwa taarifa zaidi ni vema mwandishi wa Habari hizi akawasiliana na Mkuu wa wilaya ya Rufiji kwa ajili ya kupata ridhaa ya kuchukua taarifa ndani ya wilaya yake.
Kauli ya Mke wa Kigogo
Kwa upande wake Mke wa Kigogo aliyehusishwa kuwa nyuma ya Mchakato wa Ugawwaji rushwa alizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya simu na kuelezwa kuwa ametajwa kutuma watu wagawe rushwa ya kanga na fedha,alisema suala hilo ndiyo kwanza amelisikia kutoka kwa waandishi na kwamba wakati huo alikuwa Mwanza kwa shughuli zake binafsi.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani,alipopigiwa simu kwa ajili ya ufafanuzi wa tukio hilo la Ikwirir,aliomba mwandishi ampe muda atamrudia na baada ya muda alipiga simu na kukataa kuwepo kwa watu walioshikiliwa wala kuhojiwa na taasisi hiyo.
0 Comments