DOYO ASISITIZA AMANI TANZANIA



Kigamboni, Dar es Salaam 

Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa katika kampeni zake katika mkoa wa Dar es Salaam, wilaya ya Kigamboni, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na ustawi wa taifa.

Mhe. Doyo amewaomba wananchi wa Kigamboni na Watanzania kwa ujumla kutunza amani ya nchi yetu, akisisitiza kwamba bila kujali dini, kabila, au chama cha siasa, kila Mtanzania ana jukumu la kulinda amani.

Ameonya juu ya mienendo ya uchochezi isiyo na manufaa kwa mustakabali wa taifa, akisema.
 
“Kuna haja ya kuwapuuza watu wanaohamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii. Hali kama hiyo ni hatari sana kwa mustakabali wa amani ya taifa letu. Tukio dogo linaweza kuonekana la kawaida, lakini athari zake zinaweza kuathiri maisha ya wananchi kwa miaka mingi, hata zaidi ya sita.”

Mhe. Doyo amesema kuwa amani ni msingi wa maendeleo. Amani inalinda maisha, familia, uwekezaji, elimu, na ustawi wa kila Mtanzania. Kila mmoja anatakiwa kuchukua hatua za kuepuka vurugu, kuzungumza kwa heshima, na kushirikiana kwa amani katika mijadala ya kisiasa. Hii ndiyo njia thabiti ya kuhakikisha maendeleo, demokrasia imara, na ustawi wa taifa vinadumishwa.

Historia ya nchi jirani kama Burundi, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetufundisha jinsi vurugu za kisiasa zinavyoweza kuharibu maisha ya wananchi, kuathiri familia, na kusababisha migogoro isiyoisha. Kurejesha na kudumisha amani ni jukumu letu sote, na ni faida kwa kila Mtanzania, kwani inalinda maisha, familia, uwekezaji, elimu, na ustawi wa taifa kwa ujumla.

Mhe. Doyo amewataka Watanzania kupima faida na hasara ya kila ushawishi unaotolewa na watu ambao baadhi yao familia zao zipo nje ya nchi, wanaotumia mitandao ya kijamii kujaribu kuingilia haki za watu wengine, hasa maamuzi ya kupiga kura. Amesema watu hao huwashawishi baadhi ya wananchi wasio na uelewa wa kutosha, hasa vijana, na kwamba makundi hayo ya mtandaoni yanaweza kuhatarisha amani na kuingiza taifa katika migogoro isiyo na manufaa.

Kwa upande wake, Mhamasishaji wa Kampeni wa NLD, Bi. Adija Dikulumbali, amewaonya Watanzania kwa kusema kuwa amani ikitoweka, wananchi wote, hususan kina mama, watoto, na watu wenye uhitaji maalum kama walemavu, ndio watakaoathirika zaidi. 

“Ni busara kwenda kupiga kura kwa amani na kumchagua Mhe. Doyo Hassan Doyo ili aweze kushughulikia changamoto za Watanzania kwa uadilifu. Jiunge na NLD, jitokeze kupiga kura kwa amani ili tulete mabadiliko,” alisema Bi. Dikulumbali.

Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Vijana Taifa wa NLD, Bi. Sabra Anthony Massanza, amewataka vijana waepuke kuwa daraja la wanasiasa wasio waadilifu.

“Siasa inahitaji watu waadilifu, wenye hekima na busara ili kuokoa taifa, hasa linapokumbwa na changamoto za kutokuelewana. Tusiwape nafasi wanasiasa waliopoteza hoja, na wenye malengo ya kuwatumia vijana kuleta machafuko. Watanzania, tumchague Mhe. Doyo Hassan Doyo kwa busara, kwani kuna maisha baada ya uchaguzi,” alisema Massanza.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa NLD, Bw. Don Waziri Mnyamani, ametoa wito kwa wananchi wote kujipanga na kushiriki katika uchaguzi kwa amani.

Amesema kila chama kimepewa nafasi ya kushiriki uchaguzi huu kwa hiari, na kwamba kushiriki au kutoshiriki ni haki ya kikatiba ya kila chama, haki ambayo ndiyo kiini cha demokrasia.

“Watanzania jitokezeni kupiga kura Oktoba 29. Tumchague Mhe. Doyo Hassan Doyo kwa Amani, ili akachochee Maendeleo, kwa Watanzania wote!

Post a Comment

0 Comments