TARURA KIBITI YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA UJENZI WA BARABARA NA MADARAJA


Na Miraji Msala, Kibiti – Pwani

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kibiti umeendelea kusimamia kwa karibu miradi ya barabara na madaraja, ambapo miradi mitatu iliyotekelezwa imekamilika kwa asilimia 100. Hii ni hatua muhimu inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kurahisisha maisha ya wananchi wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kibiti, Mhandisi Frederick Isangura, alisema kukamilika kwa miradi hiyo ni matokeo ya usimamizi thabiti, uwajibikaji wa wataalamu, na upatikanaji wa fedha kwa wakati kutoka Serikali Kuu.

Miradi hii ni ushahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kikamilifu kwenye sekta ya miundombinu. Upatikanaji wa fedha kwa wakati umewezesha miradi hii kukamilika kwa ufanisi na ndani ya muda uliopangwa,” alisema Mhandisi Isangura.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, miradi hiyo mitatu ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha barabara za vijijini ili kurahisisha usafiri, kuinua uchumi wa wananchi, na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo ya pembezoni mwa wilaya.

Mradi wa kwanza ni ujenzi wa barabara za Kibiti Mjini zenye urefu wa kilometa 0.6 kwa kiwango cha lami, zinazozunguka maeneo ya mji wa Kibiti. Ujenzi huo umekamilika kwa kiwango cha kuridhisha na unatarajiwa kuboresha mandhari ya mji, kurahisisha usafiri wa magari na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Mradi wa pili ni ujenzi wa Daraja la Usimbe lenye urefu wa mita 15, lililoko katika barabara ya Kipoka–Usimbe. Daraja hilo liligharimu Shilingi 258,689,200.00 na lilitekelezwa ndani ya siku 180. Kukamilika kwake kumetatua changamoto ya mawasiliano ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakikatika nyakati za mvua kutokana na maji kujaa na kukata njia.

Mradi wa tatu ni ujenzi wa barabara ya lami Majenda–Nyambangala yenye urefu wa mita 900, kwa gharama ya Shilingi 474,993,500.00, ikihusisha pia ujenzi wa makaravati, mifereji ya maji na taa za barabarani. Barabara hiyo sasa imeongeza urahisi wa kufika katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na maeneo jirani.

Mhandisi Isangura aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, zaidi ya Shilingi bilioni 10 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu wilayani Kibiti, jambo linaloendelea kubadilisha sura ya wilaya hiyo na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Bi. Asha Juma, mkazi wa kijiji cha Usimbe, alisema daraja jipya limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo, hasa nyakati za mvua.

Zamani tulikuwa tunashindwa kuvuka upande wa pili, watoto walikuwa wanakosa shule wakati wa mvua nyingi. Sasa hivi daraja limejengwa vizuri, tunapita muda wote bila shida. Tunamshukuru sana Rais Samia na TARURA kwa kutukumbuka,” alisema Bi. Asha kwa furaha.

Kwa ujumla, kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kukuza biashara ndogo ndogo, na kuboresha maisha ya wakazi wa Kibiti na maeneo jirani. Hii ni ishara kwamba TARURA inaendelea kwa karibu kusimamia utekelezaji wa miradi mipya ya barabara na madaraja wilayani humo, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa katika kubadilisha sura ya wilaya hiyo.

Post a Comment

0 Comments