KAZIINAONGEA
Dar es Salaam
Mratibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) ambaye pia ni Balozi wa Amani wa Taasisi ya Wanawake nchini Korea Kusini, Fatma Fredrick Kikkides, ametoa wito kwa vijana nchini kuhakikisha wanailinda amani ya Tanzania na kutokubali kudanganywa na taarifa potofu zinazozagaa mitandaoni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kupitia Televisheni ya Taifa (TBC2) Oktoba 23, 2025, Kikkides amesema kundi la vijana ndilo nguzo kuu ya Taifa, hivyo linapaswa kuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani, upendo na mshikamano uliopo.
“Vijana ni nguvu kazi ya Taifa. Amani tuliyonayo ni matokeo ya juhudi za vizazi vilivyotutangulia, hivyo ni jukumu letu sote kuilinda na kuiendeleza kwa manufaa ya kesho,” amesema Kikkides.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kujitambua na kuacha kufuata mikumbo ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kupandikiza chuki na kuvuruga utulivu wa nchi.
“Nawaomba vijana watambue kuwa amani inaanzia kwenye nafsi, nyumbani na sehemu za kazi. Tuilinde kwa vitendo, tusiruhusu hisia au hasira zitupeleke kupoteza misingi tuliyojengewa. Tuipeleke Tanzania yenye amani kwa kizazi kijacho,” ameongeza.
Kikkides amefafanua zaidi kuwa changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi ni ukosefu wa elimu kuhusu thamani ya amani, jambo linalowafanya baadhi kujiingiza katika makundi yenye mitazamo hasi kutokana na hasira za kukosa ajira au kukata tamaa.
“Ni muhimu sana vijana wapate elimu kuhusu amani, wajue kuwa siyo maneno tu bali ni mfumo wa maisha. Wengi wanapotea kwa sababu hawana maarifa ya kujitambua, hawajui namna ya kushiriki kujenga badala ya kubomoa,” amesema.
Akitolea mfano nchi nyingine zilizokumbwa na migogoro, Kikkides amesema vijana wengi katika mataifa hayo walishindwa kutambua thamani ya amani mapema, na walipojifunza ilikuwa ni baada ya machungu makubwa.
“Tuchukue somo hilo kabla halijatufika. Tanzania imebarikiwa utulivu wa kipekee barani Afrika. Hii ni hazina ambayo kila kijana anatakiwa kuilinda kwa maneno na matendo,” amesisitiza.
Aidha, amehimiza viongozi wa jamii, wazazi na taasisi za elimu kushirikiana katika kuelimisha vijana juu ya jukumu lao katika kudumisha amani, akisema kuwa kizazi cha sasa kinahitaji malezi yenye misingi ya uzalendo na nidhamu ya uraia.
“Elimu ya amani inaanzia nyumbani. Wazazi wawafundishe watoto kuheshimu, kujadiliana kwa hoja, siyo kwa matusi au hasira. Shuleni tuwafundishe uzalendo na wajibu wao kwa nchi. Tukifanya hivyo, tutakuwa na kizazi kinachoilinda amani kwa hiari, si kwa kulazimishwa,” ameeleza Kikkides.
Akizungumza kuhusu mitandao ya kijamii, ametahadharisha kuwa japokuwa teknolojia imeleta fursa nyingi, imekuwa pia uwanja wa kusambaza chuki na taharuki, hasa nyakati za kisiasa.
“Mitandao ya kijamii ni kama moto, inaweza kupika chakula au kuchoma nyumba. Ni lazima vijana wawe na busara katika matumizi yake. Watumie mitandao kujenga, kuelimisha, na kuleta matumaini, si kubomoa,” amesema kwa msisitizo.
Kikkides amehitimisha kwa kutoa wito wa kitaifa kwa vijana wote kushirikiana kulinda amani, bila kujali itikadi, dini au kabila, akisisitiza kuwa Tanzania ni moja na itabaki kuwa hivyo iwapo kila mmoja atachukua jukumu lake.
“Amani si jukumu la serikali pekee. Ni jukumu la kila mmoja wetu. Tukianza sisi vijana, tutakuwa tumetengeneza kizazi cha matumaini na Taifa lenye heshima duniani,” amesema kwa kujiamini.
Kauli ya Kikkides inajidhihirisha kuwa ni mwendelezo wa wito wa viongozi mbalimbali wanaohamasisha kulinda amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Wito huo umekuwa ukisisitiza mshikamano, nidhamu na uzalendo kama dira kuu ya Tanzania.
“Amani ni urithi wetu — tuilinde kwa vitendo.”
#DumishaAmaniKupigaKuraniHakiYako

0 Comments