Serikali ilivyobadili sura ya ajira, maslahi watumishi wa umma



NA MWANDISHI WETU 

KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya utumishi wa umma imepiga hatua katika kuboresha maslahi, ustawi na mazingira ya kazi ya watumishi wa umma nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, serikali imeweka msukumo maalum kuhakikisha watumishi wanathaminiwa, wanalindwa na wanapata haki zao kwa wakati.

MASLAHI YABORESHWA

Waziri Simbachawene anasema Rais Samia amefanya mageuzi makubwa katika eneo la maslahi ya watumishi wa umma. Miongoni mwa hatua hizo ni kupunguza Kodi ya Mshahara (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane, na kuongeza kiwango cha chini kinachotozwa kodi kutoka Sh. 170,000 hadi Sh. 270,000. Hatua hiyo imewezesha serikali kuwasamehe watumishi kodi yenye thamani ya Sh. bilioni 14.78.


Vilevile, Waziri Simbachawene anasema serikali imefuta tozo ya asilimia sita (retention fee) iliyokuwa ikikatwa kwa watumishi waliokuwa wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu, jambo lililowaongezea watumishi hao unafuu wa jumla ya Sh. trilioni 1.1.

Katika sekta ya afya, serikali imepanua wigo wa wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa kuongeza umri wa watoto wategemezi kutoka miaka 18 hadi 21, hatua iliyowanufaisha watoto 65,353 kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 3.7.

Serikali pia imeongeza viwango vya posho za kujikimu na imepandisha mishahara kwa asilimia 23.3, huku nyongeza za mwaka (annual increment) zikitolewa kwa mujibu wa taratibu.

 

ULIPAJI MADENI

Kuhusu ulipaji madeni ya mishahara, Waziri Simbachawene anasema kuwa hadi Machi 31, 2025, serikali ilikuwa imeshughulikia madai ya watumishi 130,463 yenye jumla ya Sh. bilioni 226.5, na malimbikizo ya wastaafu 10,022 yenye thamani ya Sh. bilioni 33.2.


Katika kipindi hicho hicho, watumishi 610,733 wamepandishwa vyeo, 42,515 wamebadilishwa kada na huku 133,317 wakiajiriwa upya katika taasisi mbalimbali za umma. Serikali pia imetoa vibali 39,934 vya ajira mbadala.

Waziri huyo anasema serikali imeanzisha Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal) unaowawezesha watumishi kupata huduma zao za kiutumishi bila kulazimika kufika ofisini.

Kupitia mfumo huo, watumishi wanaweza kuomba likizo, uhamisho, mikopo, kubadilishana vituo vya kazi na hata kuona hati zao za mishahara kwa urahisi.

AJIRA MPYA

Ili kukabiliana na upungufu wa watumishi, Waziri Simbachawene anasema serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira imetoa jumla ya ajira mpya 55,162 katika kipindi cha miaka minne. Idadi ya walioajiriwa imeongezeka kutoka 7,659 mwaka 2020 hadi 20,158 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 163.


Waziri Simbachawene anasisitiza kuwa mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya Rais Samia kuimarisha utawala bora na kuifanya serikali kuwa ya kidijitali, yenye uwazi na inayowajali watumishi wake.

“Rais Samia ameweka msingi thabiti wa utumishi wa umma unaojali utu, maslahi na weledi. Huu ni ushahidi wa serikali sikivu na inayotenda,” anasema Simbachawene.

Kwa ujumla, Waziri Simbachawene anasema miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa kipindi cha mageuzi chanya katika historia ya utumishi wa umma nchini, ikilenga kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na ustawi wa mtumishi wa umma kwa manufaa ya taifa zima.

KAULI YA SAMIA

Kupitia hotuba yake ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 jijini Dodoma, Juni 27, 2025, Rais Samia aliweka wazi mafanikio makubwa ya serikali yake katika kukuza ajira na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

Alieleza kuwa kati ya mwaka 2020 hadi 2025, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imezalisha ajira 8,084,204 kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi. Hii ni moja ya hatua za mafanikio makubwa ya Serikali katika kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza tija kwa nguvu kazi ya taifa.

“Tutazidi kuwekeza kwenye sekta zenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi, kwani nguvukazi kubwa tuliyonayo ni mtaji muhimu wa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Rais Samia, akisisitiza dhamira ya serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji wenye tija.

THAMANI YAO

Katika sekta ya utumishi wa umma, Rais Samia alisema serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha watumishi wanathaminiwa na kupewa mazingira bora ya kazi.

Alibainisha kuwa jumla ya watumishi 611,063 wamepandishwa vyeo, 42,557 wamebadilishwa kada na 9,620 wamefanyiwa mabadiliko ya mishahara binafsi. Aidha, watumishi wapya 135,626 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali za umma.

Serikali pia imeongeza mshahara wa kima cha chini kutoka Sh. 370,000 hadi Sh. 500,000, ongezeko la asilimia 35.1, ikiwa ni dalili ya kujali ustawi wa mtumishi.

Vilevile, jumla ya Sh. bilioni 252.76 zimelipwa kwa watumishi 150,647 waliokuwa na madai ya mishahara na Sh. bilioni 33.29 zimelipwa kwa wastaafu 10,022.

Rais alisema hatua hizi zimeimarisha ari ya watumishi, uwajibikaji na heshima kwa serikali, huku huduma kwa wananchi zikipata ufanisi mkubwa.

USIMAMIZI WAO

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene, serikali imeanzisha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu (HR-Assessment) ili kuondoa changamoto ya upungufu wa watumishi katika maeneo mbalimbali. Mfumo huo unasaidia kubaini idadi ya watumishi waliopo, upungufu na ziada katika kila kituo cha kazi.

Hadi Mei 2024, mfumo huo umehusisha mikoa yote 26 na taasisi 534 za umma, ukionesha kuwa kati ya watumishi 597,396 waliopo, bado kuna upungufu wa 441,366.

Kupitia mfumo huo, serikali imepata picha kamili ya mahitaji ya rasilimali watu, jambo litakalorahisisha upangaji ajira mpya kulingana na vipaumbele vya maendeleo.

DIRA YA AJIRA

Katika sekta ya utumishi, Rais Samia alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ya biashara, uwekezaji na utumishi bora wa umma ili kuchochea ukuaji wa ajira endelevu.

“Hatutapumzika hadi kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi apate fursa ya kujipatia kipato halali kupitia kazi. Huu ndiyo msingi wa ustawi na maendeleo ya kweli,” alisema Rais Samia.

KAULI YA TUCTA

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kupitia Rais wake, Tumaini Nyamhokya, linapongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza hatua 16 muhimu zilizolenga kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi.

Nyamhokya anasema hatua hizo ni kielelezo cha dhamira ya Rais Samia kulinda hadhi ya wafanyakazi nchini. Miongoni mwa mafanikio hayo ni nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 na sekta binafsi kwa asilimia 34.4, pamoja na kupunguzwa kwa Kodi ya Mishahara (PAYE) kutoka asilimia tisa (9) hadi nane (8).

Mafanikio mengine ni kuongezwa kwa umri wa mtoto mnufaika wa NHIF kutoka miaka 18 hadi 21, kuondolewa kwa tozo ya asilimia sita kwenye mikopo ya elimu ya juu, na ongezeko la posho za kujikimu, muda wa ziada na za kuitwa kazini. 

Anasema serikali pia imepandisha kima cha chini cha pensheni kutoka Sh.100,000 hadi Sh.150,000, kuanzisha nyongeza ya kila mwezi ya pensheni kwa asilimia mbili na kupandisha kikokotoo cha mafao ya mkupuo hadi asilimia 40.

Vilevile, Nyamhokya anasema serikali imeajiri watumishi wapya, imepandisha madaraja kwa zaidi ya watumishi 412,000 na kuboresha mifuko ya hifadhi ya jamii, hatua iliyosaidia wastaafu kulipwa kwa wakati. 

Alisema TUCTA inatambua ushirikiano wa karibu na serikali kupitia kamati ya UTATU na Bodi ya Kima cha Chini, akitoa wito kwa waajiri kutekeleza nyongeza hizo kwa haki.

WATUMISHI WALONGA

Si viongozi wa serikali pekee wanaoona matunda ya jitihada hizi, bali pia watumishi wenyewe wameshuhudia mabadiliko makubwa.

Mwalimu Daudi Bukela, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masunula, katika kata ya Usule wilayani Shinyanga, anasema hatua za serikali zimemaliza changamoto za muda mrefu.

“Walimu tumepandishwa madaraja na mshahara. Kwa waliostahili, wote wamepanda. Katika miaka hii minne ya uongozi wa Rais Samia, ameboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kujenga miundombinu na kuongeza watumishi shuleni. Hapa Masunula nimeongezwa mwalimu mmoja, sasa tuko walimu wanane kwa wanafunzi 620,” anasema Mwalimu Bukela.

Kwa upande wake, Mwalimu Chausiku Shaban anasema hatua zilizochukuliwa na serikali zimeleta heshima na ari mpya kwa watumishi wa umma.

“Tumepandishwa madaraja. Ni haki ya mtumishi, lakini haikutolewa huko nyuma. Tumeongezwa mishahara, tumepata mafunzo yanayojumuisha shule salama – maadili ya walimu na wanafunzi shuleni na nje ya shule, na hii imetolewa nchi nzima.

“Pia tumepatiwa mafunzo kuhusu mtaala mpya wa elimu, jambo lililotuwezesha kuelewa kilichobadilika. Hapa kwetu Shule ya Msingi Tabu Hotel (Halmashauri ya Wilaya ya Gairo), tumepata madarasa manne mapya,” anasema Mwalimu Chausiku.

Post a Comment

0 Comments