UWT YAWAFIKIA WANAWAKE WAPIGA KURA MILIONI 15 JIJINI DAR ES SALAAM, lengo ni kupata Wapiga Kura Zaidi Kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29





KAZIINAONGEA

Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amesema hadi kufikia jana Oktoba 22, umoja huo kwa kushirikiana na kamati mbalimbali za kanda jijini Dar es Salaam, umefanikiwa kuzungumza na wanawake milioni 15 katika kampeni za uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya taifa na uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza Oktoba 23, 2025 jijini Dar es Salaam, Chatanda amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa UWT kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa, huku akisisitiza kuwa kazi hiyo bado inaendelea kwa kasi kubwa.

“Tumefanikiwa kufikia wanawake milioni 15 mpaka jana, na tunalenga kufikia wanawake milioni 17 wa Dar es Salaam kabla ya kumalizika kwa kampeni hizi. Tuna hakika wanawake wataendelea kuwa nguvu ya ushindi wa maendeleo,” amesema Chatanda.

Ameongeza kuwa kampeni hizo zimehusisha mikutano ya hadhara, vikao vya vikundi vya kiuchumi, na mikakati ya uhamasishaji kupitia mitandao ya kijamii, yote yakilenga kumuinua mwanamke kiuchumi na kumtia moyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Chatanda amesisitiza kuwa UWT itaendelea kuwa chombo thabiti cha kuwakilisha maslahi ya wanawake, kuhakikisha wanapata nafasi sawa katika fursa zote, na kwamba kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha mshikamano, ubunifu na ujasiri wa wanawake wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya chama katika kuhakikisha ushirikiano wa karibu kati ya wanawake wa mijini na vijijini unaimarishwa, huku wakipewa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi yanayohusu maisha yao.

Post a Comment

0 Comments