GHARAMA YA VURUGU: TUSIACHE WACHACHDE WAHARIBU AMANI YA WENGI







Na Mwandishi Wetu

Tanzania, taifa lililojijengea heshima kubwa kwa amani na utulivu wake katika bara la Afrika, lilishuhudia Jumatano Oktoba 29, 2025, tukio lisilotarajiwa la machafuko katika baadhi ya maeneo, hasa katika majiji na miji mikubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Wakati mamilioni ya wananchi wakijitokeza kwa utulivu kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani pamoja na wawakilishi kwa upande wa Tanzania Zanzibar, kundi la watu wachache lilitumbukia katika vitendo vya uvunjifu wa amani, likivamia vituo vya kupigia kura, kufanya uporaji madukani na kuharibu mali za watu.

Matukio hayo yalisababisha hofu, uharibifu wa mali, majeruhi na hata vifo katika baadhi ya maeneo, ingawa bado hakuna taarifa rasmi ya serikali kuhusu hali ya majeruhi na idadi ya vifo.

Hali hiyo ililazimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura, kutangaza marufuku ya watu kutokuwa barabarani kuanzia saa 12:00 jioni, isipokuwa wale waliokuwa kwenye majukumu rasmi ya ulinzi na usalama. Ni hatua nzito, lakini yenye lengo la kulinda maisha ya watu na kuzuia madhara zaidi.

MADHARA SI YA LEO TU

Vurugu, hata kama zinatokana na kundi dogo la watu, huacha makovu makubwa katika jamii. Kwanza, uchumi wa wananchi unapoteza mwelekeo. Maduka yaliyovunjwa Oktoba 29 na siku zilizofuata ni vyanzo vya kipato kwa familia nyingi, wazazi waliokuwa wanategemea biashara hizo kulipa ada za shule, kulisha familia au kulipa kodi sasa wamebaki mikono mitupu.

Pia, vituo vya mafuta vilivyoharibiwa ni kiungo muhimu cha shughuli za kila siku. Leo, magari mengi yamesimama na wasafiri wamekwama.

Usafiri wa majini kama Dar es Salaam, uliokuwa tegemeo kuu kwa maelfu ya wakazi wanaoishi Kigamboni, Kivukoni na maeneo mengine, ulisitishwa kwa muda kutokana na vurugu hizo. Waliokuwa wanakwenda hospitalini, hasa wagonjwa wa dharura, walijikuta katika hali ya majonzi na hofu.

Athari hizo zimefika hata kwenye sekta ya elimu na utumishi wa umma. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk/. Moses Kusiluka, alilazimika kutoa tamko rasmi, akiwataka watumishi wa umma kufanya kazi kutoka nyumbani na wanafunzi kubaki majumbani. Ni hatua ya tahadhari, lakini pia ni kielelezo cha jinsi vurugu zinavyoweza kusimamisha maisha ya taifa lote.

Ni ukweli mchungu kwamba katika kila fujo, hakuna mshindi. Hasara haibagui chama, dini wala kabila. Wale waliopoteza ndugu, jamaa au marafiki katika vurugu hizo hawataweza kupata faraja kwa matokeo yoyote ya kisiasa.

Uharibifu wa mali za umma, kama vituo vya kupigia kura, magari ya umma na miundombinu, ni hasara ya taifa zima. Serikali italazimika kutumia fedha za walipakodi kurekebisha yaliyovunjwa, badala ya kuelekeza rasilimali hizo katika huduma za jamii kama elimu na afya.

Huu ndio ukweli usiopingika; vurugu zinaharibu maisha ya watu wa kawaida zaidi ya wale wanaozianzisha. Wale wanaoanzisha fujo mara nyingi hawana chochote cha kupoteza, lakini madhara yake huwakumba hata wale wasiokuwa na hatia.

Wito wa IGP Wambura wa kutokuwa barabarani baada ya muda tajwa haukuwa adhabu, bali ni hatua ya kiusalama yenye lengo la kuokoa maisha. Ni muhimu wananchi waelewe kuwa katika mazingira kama haya, usalama wa taifa ni jukumu la pamoja. Kutii maagizo ya vyombo vya dola ni ishara ya uzalendo na heshima kwa taifa.

Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vinafanya kazi katika mazingira magumu kuhakikisha vurugu hazisambai zaidi. Wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa za wahalifu, kutoshiriki katika uvunjaji sheria na kuzuia wimbi la upotoshaji mitandaoni linaloweza kuchochea taharuki zaidi.

HASARA YA KIJAMII

Vurugu si tu zinaharibu mali na kuua, bali zinavunja misingi ya imani na mshikamano wa kijamii. Watu wanapopoteza imani kwa wenzao au taasisi za serikali, urejeshaji hali ya kawaida unakuwa mgumu zaidi. Ni wajibu wa viongozi wa dini, wazee wa mila na asasi za kiraia kusimama kidete kupaza sauti za busara, kuhimiza maridhiano na kujenga tena imani miongoni mwa wananchi.

SOMO KWA TAIFA

Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa utulivu wake wa kisiasa kwa miongo kadhaa. Ni vyema tukumbuke kuwa amani tuliyo nayo si bure, ni matokeo ya kazi ya vizazi vilivyotutangulia, vilivyolinda heshima na utu wa taifa hili. Tukiruhusu vurugu kutawala leo, tutakuwa tunavunja msingi uliotuwezesha kufika hapa.

Ni muhimu kujifunza kutokana na yaliyotokea Oktoba 29 na siku zilizofuata. Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote wanapaswa kufanya tathmini ya kina juu ya nini kilisababisha vurugu hizo, ili hatua za haraka zichukuliwe kuzuia kurudiwa kwa makosa hayo.

Matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuata yanatukumbusha kuwa amani ni urithi wa thamani unaoweza kupotea ndani ya dakika chache. Vurugu hazijawahi kuwa suluhisho la kisiasa. Zinaleta maumivu, huzuni na hasara ya vizazi.

Leo tunapoamka katika utulivu wa tahadhari, ni lazima tujiulize: “Ni nini tunataka kuacha kwa watoto wetu - taifa lenye heshima au lililogawanyika kwa hasira za wachache?”

Tuchague hekima badala ya hasira, utulivu badala ya vurugu na ujenzi wa taifa badala ya uharibifu. Tanzania ni yetu sote na jukumu la kuilinda ni letu sote.

Post a Comment

0 Comments