MBETO: RAIS MWINYI, SAMIA WAMEAPA KUWALINDA WATANZANIA


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekula kiapo cha kuwalinda waTanzania kwa mujibu wa katiba hivyo wananchi wasikubali kuyumbishwa na wachochezi wa uvunjifu wa amani wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake, CCM Kisiwandui leo 06 Novemba 2025, Katibu wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema viongozi hao wa nchi ni wajibu wao na ndicho wanachofanya kuwalinda na kulinda utu wao dhidi wasioitakia mema nchi.

"Viongozi wetu wanatekeleza takwa la kikatiba na wananchi wanapaswa kujiepusha na aina zozote za uvunjifu wa amani wakati hatua zaidi zikichukuliwa dhidi ya wale waliochochea na kuhusika na vurugu za 29 Oktoba 2025" alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa amani ni tunu ya Taifa na ni wajibu wa kila mmoja kuilinda na nchi haitashurutishwa na mtu au kikundi cha nje au ndani na mataifa ya kigeni katika kutekeleza mambo yake.

Mwenezi Mbeto aliwaasa hususan vijana kukataa kutumika kuvuruga amani na kusababisha uharibifu wa mali kwani tunu hiyo ikipotea ni ngumu kuirudisha.

Mbeto pia alitumia fursa hiyo kuwapongeza Rais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi kwa ushindi wa kishindo walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita ambao unaonyesha jinsi waTanzania walivyo na imani nao.

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan alishinda kwa zaidi ya asilimia 97 na mgombea nafasi ya Rais Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliibuka na ushindi wa asilimia 74.08.

Post a Comment

0 Comments