*Yaibugiza Mabao Matatu Kwa Nunge
Na Beatus Maganja, Morogoro
Kikosi cha timu ya mpira wa miguu cha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kimeendelea kuonesha ubabe wake kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) baada ya leo Novemba 28, 2025 kutamba kwa ushindi mnono wa mabao 3–0 dhidi timu ya Bandari katika mtanange uliochezwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kiislamu (Muslim University) Mkoani Morogoro.
Mithili ya Mbogo aliyejeruhiwa, TAWA ilianza kipindi cha kwanza kwa kasi huku wakitengeneza mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la timu ya Bandari yaliyopelekea CR II Dismas Kakulu kuangushwa ndani ya eneo la penati na mwamuzi bila kusita akaelekeza adhabu ya penati iweze kutolewa dhidi ya Bandari.
Bila ajizi CR II Ismail Omary aliachia shuti kali kama vile ngiri achomokavyo kutoka katika shimo lake na kukwamisha mpira kimiani na hivyo kuifanya TAWA iongoze Kwa bao la kwanza.
Kipindi cha pili kilipoanza, TAWA walirudi na nguvu mpya ambapo dakika ya nane ya mchezo, CR II Dismas Kakulu aliyekuwa mwiba mkali muda wote katika mchezo huo alipokea pasi safi kutoka kwa Kapteni wa timu hiyo PC Carlos Mbilo na kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Bandari ambaye pamoja na kuruka Kwa umahiri mithili ya nyumbu "mwongoza watalii" anayepatikana Tabora Zoo aliambulia patupu na hivyo TAWA kuandika bao la pili.
Bandari wakijaribu kurejea mchezoni, TAWA waliendelea kusukuma "ngozi" kwa kasi ambapo dakika ya 15 CR III Bilasa Marius akiwa ndani ya eneo la upande wa kulia wa kipa, alikamata mpira na kukomelea shuti lililomwacha kipa wa Bandari akitazama nyavu huku akishika mikono kiunoni na hivyo kufunga ukurasa wa magoli.
Katika mechi ya leo, TAWA walitawala mchezo kuanzia kipindi cha kwanza wakionesha nidhamu, ufundi, mbinu, na kasi ya hali ya juu. Ushindi huu unaibakiza timu hiyo katika nafasi nzuri zaidi kwenye mbio za kutinga hatua inayofuata ya michuano ya SHIMMUTA 2025.



0 Comments