WAZIRI KAPINGA: FCC YAFANYA KAZI KUBWA KULINDA WALAJI NA KUDHIBITI BIDHAA FEKI



Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa kufanya kazi kubwa katika kusimamia ushindani, kulinda walaji na kupambana na bidhaa feki, huku ikitoa elimu kuhusu masuala ya kibiashara pamoja na kuhusisha uchambuzi wa miunganiko ya makampuni makubwa ili kuhakikisha ushindani wenye manufaa kwa taifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za FCC, Waziri Kapinga alisema ziara hiyo ya Desemba 24, 2025 imelenga kuimarisha misingi ya utendaji na kuongeza ufanisi wa tume hiyo.

“Tunahitaji kuhakikisha watanzania—ambao ndio walaji wetu na wateja wakuu—wanapata huduma bora. Kikao cha leo kinalenga kuboresha utendaji kazi, kuongeza njia za kuwafikia walaji na kupata mrejesho wa kazi tunazofanya kwa urahisi zaidi,” alisema Kapinga.

Ameongeza kuwa wizara yake itaendelea kuisimamia FCC kuboresha mbinu za udhibiti, kupambana na bidhaa feki na kukuza ubunifu ili kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, Hadija Juma Kasongwa, alisema tume inaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, inayolenga kutatua changamoto za wananchi, hususan katika mazingira ya biashara.

Bi. Kasongwa alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imewekeza katika mazingira ya kukuza uwekezaji, na FCC imekuwa ikipitia na kuchambua miamala ya muunganiko wa makampuni kwa lengo la kukuza mitaji na kuokoa ajira katika kampuni na viwanda mbalimbali.

Aidha, alitangaza kuwa kuanzia Desemba 1, 2025, kutakuwa na zoezi maalumu la kurekodi usafirishaji wa bidhaa zote zinazoingia nchini, lengo likiwa ni kuimarisha uchunguzi na kudhibiti bidhaa feki na zile zisizokidhi viwango.

Post a Comment

0 Comments