NA ABRAHAM NTAMBARA
Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Salum Kalli ameagiza wakuu wa shule wilayani humo kutomzuia mwanafunzi kuanza masomo kwa sababu yoyote ile shule zitakapofunguliwa Januari 13, 2026.
Kauli hiyo ya Mhe. Kalli imekuja siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, kuwaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha hakuna mtoto anayezuiwa kuanza au kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa sare, wakati shule zote nchini zitakapofunguliwa.
Mhe. Kalli akizungumza leo Disemba 31, 2025 akiwa katika Shule ya Sekondari ya Kimokouwa wakati wa hitimisho la ziara ya siku mbili ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longodo Mhe. Thomas Ngobei ya kukagua maandalizi ya upokeaji wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, Awali na Darasa la Kwanza kwa muhula wa masomo wa mwaka 2026.
DC Kalli amesema kuwa amepokea agizo hilo la Waziri Shemdoe, hivyo atasimamia na kuhakikisha hakuna mtoto anayekwamishwa kuanza au kuendelea na masomo shule zitakapofunguliwa.
“Nimepokea agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe. Nimhakikishie hakuna mwanafunzi atakayezuiwa masomo kwa sababu ya kokosa Sare. Na mimi niagize Walimu Wakuu wasimzuie Mwanafunzi yeyote kwa sababu ya kukosa sare,” amesema Mhe. Kalli.
Hivyo Mhe. Kalli ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shule zitakapofunguliwa.
Katika hatua nyingine wakati tukiaga Mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026, DC Kalli ametumia fursa hiyo kwa kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ya Wilaya ya Longido ikiwemo miradi ya Elimu, Maji, Afya na Barabara.
Amesema kuwa katika mwaka huu Shule sita zimejengwa ambazo kila moja imegharimu Zaidi ya shilingi milioni 580, kadhalika amefanikisha vijiji vyote vya Wilaya ya Longido kufikiwa na huduma ya umeme huku vitongoji Zaidi ya asilimia 84 vikifikiwa na nishati hiyo.
0 Comments