Mazingira ya uwekezaji, kasi ya utoaji leseni na usalama yaimarika
Wachimbaji vijana wahamasisha vijana wengine kuchangamkia fursa
Katavi, Desemba 02, 2025
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Andrew Mwalugaja amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa katika Sekta ya Madini, akibainisha kuwa mkoa huo umebahatika kuwa na rasilimali za madini ikiwemo dhahabu, shaba, risasi, fedha, nikeli, manganese na madini ya ujenzi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Mhandisi Mwalugaja amesema ofisi yake imeendelea kuongeza ushiriki katika Sekta ya Madini kupitia utoaji leseni mpya, ikiwemo leseni tatu za utafiti katika mwaka wa fedha 2025/2026 kati ya Julai na Oktoba 2025 katika Wilaya za Mpanda, Tanganyika na Mlele, leseni 19 za uchimbaji wa kati, pamoja na leseni 290 za uchimbaji mdogo.
Ameongeza kuwa utoaji wa leseni za biashara ya madini nao umeimarika, ambapo mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya leseni 107 zilitolewa, 35 za biashara kubwa ya madini na 72 za biashara ndogo ya madini. Tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mapema Julai hadi Oktoba, leseni 82 za biashara ya madini zimetolewa zinazojumuisha leseni kubwa 34 na ndogo 48.
Amesema Serikali imeanzisha masoko mawili ya madini katika Manispaa ya Mpanda na eneo la Karema ili kuhakikisha wachimbaji wanapata soko la uhakika, huku mazingira ya uwekezaji yakiendelea kuimarika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kuongeza usalama na mifumo rafiki kwa wawekezaji.
Ameeleza kuwa Sekta ya Madini imeendelea kuleta mafanikio makubwa, hususan katika ongezeko la maduhuli ya Serikali kutoka Shilingi bilioni 1.16 mwaka 2017/2018 hadi Shilingi bilioni 9.26 mwaka 2024/2025. Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2025 pekee, Shilingi bilioni 3.80 tayari zimekusanywa sawa na asilimia 38 ya lengo la mwaka la Shilingi bilioni 10.
Wadau wa madini katika mkoa huo wamepongeza juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji, wakibainisha kuwa maboresho ya miundombinu, utatuzi wa changamoto kwa haraka na upatikanaji wa huduma za kiserikali kwa wakati.
0 Comments