Dar es Salaam
Umoja wa Wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam umewataka Watanzania wote kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kulivuruga taifa, ukisisitiza kuwa machafuko hayana tija wala hayatoi suluhu ya kudumu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, umoja huo umesema unapinga vikali wito wowote wa vurugu unaotolewa na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi wanaodaiwa kuwa na maslahi binafsi, huku wakilihatarisha taifa kwa kuingiza hofu na machafuko.
Wajasiriamali hao wamesema wamefuatilia kwa karibu matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kubaini kuwa kulikuwa na watu waliokuwa nyuma ya pazia wakihamasisha vitendo hivyo. Wamesisitiza kuwa wamewashtukia wahusika hao na wanapinga vikali mienendo hiyo wanayoieleza kuwa hatarishi kwa amani na ustawi wa nchi.
Kwa mujibu wa tamko lao, waathirika wakubwa wa vurugu hizo walikuwa ni wafanyabiashara, wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo ndogo, waliopata hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali pamoja na kusimama kwa shughuli za kiuchumi.
“Tutaendelea kupaza sauti kupinga uchochezi wa aina yoyote. Tutapingana na wanaharakati wanaojificha nje ya nchi kuhamasisha vurugu na maandamano. Tunakataa ushawishi wa wanamitandao wanaoeneza chuki, tutawakemea wanasiasa wanaohamasisha vurugu na pia viongozi wa dini wanaoingiza siasa katika majukwaa ya kiimani,” limeeleza tamko hilo.
Aidha, wajasiriamali hao wamesema wataendelea kuwahamasisha vijana wa kizazi cha Gen Z kuwa nguvu kazi muhimu ya taifa, na kuwajengea misingi ya kulinda amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.
Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali, Mzee Omary Suleiman, mfanyabiashara wa Soko la Kinondoni, amesema vurugu hizo zilitokana na uchochezi wa makusudi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena.
“Tanzania ni mimi, na mimi ni nchi. Tunaomba Watanzania wote waunge mkono jitihada hizi ili taifa letu libaki salama, lenye amani na utulivu,” alisema Mzee Suleiman.
Tamko hilo limekuja kufuatia ushirikiano wa Taasisi ya MICIRA, ambayo imeelezwa kutoa elimu ya uraia kwa wafanyabiashara, hatua inayochangia kuongeza uelewa kuhusu haki, wajibu na umuhimu wa kulinda amani ya taifa.
Wafanyabiashara wengine waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Husein Bambe, Kiongozi wa Wajasiriamali Ubungo; Bakari Sufia wa Ilala; na Pelagia Michael, Makamu Mwenyekiti wa Wajasiriamali Kinondoni, ambao kwa pamoja wamesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa biashara, maendeleo na ustawi wa Taifa la Tanzania.
.jpg)

0 Comments